Kampuni ya Umeme nchini ya Kenya Power (KPLC) imekanusha madai kuwa transfoma zilizoondolewa katika eneobunge la Mbeere Kaskazini zilihamishwa kwa sababu za kisiasa, ikisema hatua hiyo ilikuwa sehemu ya zoezi la kawaida la Uboreshaji linalolenga kuimarisha usalama na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Katika taarifa yake, kampuni hiyo imeeleza kuwa transfoma zinazopata hitilafu za kiufundi, ikiwemo kuingia kwa maji au matatizo mengine ambayo hayawezi kurekebishwa kwenye eneo husika, huondolewa na kupelekwa katika karakana maalum kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati na kukaushwa kwa njia maalum kabla ya kurejeshwa katika eneo lake.
Kenya Power imesema hatua hizo za uboreshaji zimechangia kupunguza kwa kiwango kikubwa hitilafu za transfoma kote nchini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, na zinaendelea kuwa sehemu muhimu ya mpango wa kampuni wa kuhakikisha huduma bora ya umeme.
“Hatua hizi za uboreshaji zimepunguza kwa kiasi kikubwa hitilafu za transfoma kote nchini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,” kampuni hiyo imesema.
Kenya Power imefichua kuwa transfoma 15 ziliondolewa katika eneobunge la Mbeere Kaskazini kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu kwa ajili ya uboreshaji wa kawaida.
Kati ya hizo, 14 tayari zimekarabatiwa na kurejeshwa katika maeneo husika, huku moja ikiharibiwa na wahalifu wiki iliyopita na inatarajiwa kubadilishwa Ijumaa, Julai 10, 2026.
“Tunawahakikishia wateja wetu kuwa shughuli hizi za uboreshaji ni za kiufundi na zinafanywa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme salama, wa kuaminika na thabiti,” ilisema Kenya Power.
Ufafanuzi huo umetolewa baada ya hofu kuibuka miongoni mwa wakazi wa Mbeere Kaskazini kufuatia kuondolewa kwa baadhi ya transfoma zilizokuwa zimesakinishwa mwaka 2025 kupitia mpango wa Last Mile Connectivity.
Kupitia mpango huo, familia nyingi ziliunganishwa na huduma ya umeme kwa mara ya kwanza baada ya kukosa umeme kwa muda mrefu.
Kuondolewa kwa transfoma hizo kuliibua maswali miongoni mwa wakazi, huku baadhi yao wakidai kuwa vifaa hivyo vilikuwa vimehamishwa hadi Ol Kalou kabla ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneo hilo.
Hata hivyo, Kenya Power imekanusha madai hayo na kusisitiza kuwa zoezi la uboreshaji wa transfoma hufanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa misingi ya kiufundi pekee, bila kuhusishwa na shughuli za kisiasa au uchaguzi.









