Rais William Ruto ametangaza msamaha wa ada za leseni za biashara kwa kipindi cha miaka miwili kwa vijana wote watakaonufaika na mpango wa NYOTA, akisema hatua hiyo inalenga kuwawezesha kuanzisha na kukuza biashara zao bila kubebeshwa gharama kubwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa kuwawezesha vijana kiuchumi wa NYOTA katika Uwanja wa Ulinzi Complex, Lang’ata jijini Nairobi, Rais Ruto amesema serikali itatumia shilingi bilioni 3 kufadhili vijana 122,000 kote nchini kupitia mpango huo.
Rais amesema tayari ameelekeza Baraza la Bajeti na Uchumi la Serikali kwa kushirikiana na serikali za kaunti kutekeleza msamaha huo wa leseni za biashara kwa wanufaika wote wa NYOTA.
“Ninaagiza Baraza la Bajeti na Uchumi la Serikali, kwa kushirikiana na serikali za kaunti, kutekeleza msamaha wa ada za leseni za biashara kwa kipindi cha miaka miwili kwa wanufaika wote wa NYOTA,” amesema Rais Ruto.
Kulingana na Rais, hatua hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya kisheria na gharama zinazowakabili wajasiriamali wachanga ili kuwapa nafasi ya kuimarisha biashara zao.
“Baada ya kuona kile ambacho vijana hawa wamefanikiwa kufanya kwa msaada mdogo walioupata, sasa ni jukumu la serikali kuondoa vikwazo vinavyowazuia.” Ameongeza Rais.
Ruto amesema mpango wa NYOTA ni sehemu ya juhudi za serikali za kujenga uchumi unaotegemea ujasiriamali, ambapo vijana watahamasishwa kuanzisha biashara badala ya kutegemea ajira pekee.
“Tunajenga Kenya ambayo ujasiriamali unathaminiwa na ambapo kila kijana anapata fursa ya kujenga biashara badala ya kutafuta ajira pekee,” amesema.
Aidha, Rais amesema biashara changa zinapaswa kupewa muda wa kukua kabla ya kubeba mzigo wa gharama zote za kutimiza masharti ya kisheria.
Pia ameiagiza Wizara ya Ushirika na iashara Ndogo Ndogo kuanzisha mfumo wa kitaifa wa utambuzi wa wanufaika wa NYOTA ili kuwawezesha kupata kwa urahisi huduma za serikali na fursa mbalimbali za kukuza biashara zao.
Kuhusu maendeleo ya miundombinu, Rais Ruto amesema Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu (NIF) itasaidia kufadhili miradi mikubwa ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu kama vile mabwawa ya maji, uwanja wa ndege, uwanja wa michezo miongoni mwa mengine.
Amesema hazina hiyo tayari ina shilingi bilioni 350, ambazo zitasaidia kugharamia miradi muhimu na kuiandaa nchi kwa mahitaji ya maendeleo ya baadaye.
Aidha, Rais Ruto amesema kuwa sheria ya Hazina ya Utajiri wa Kitaifa (Sovereign Wealth Fund) ambayo aliitia saini Jumatano tarehe 8 Julai 2026, utasaidia kukuza usawa wa vizazi kwa kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na kutumiwa kunufaisha kizazi cha sasa pamoja na vizazi vijavyo.









