Kiwanda cha Kusafisha Mafuta chake Aliko Dangote kuwaajiri Vijana Elfu 60,000.

0

Takriban vijana 60,000 wanatarajiwa kupata ajira kupitia ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Afrika Mashariki kitakachojengwa katika Kaunti ya Lamu kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kenya na mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa kuwawezesha vijana kiuchumi wa NYOTA jijini Nairobi, Rais William Ruto amesema mradi huo utabuni fursa za ajira kwa maelfu ya vijana wakati wa ujenzi na wakati wa uendeshaji wa kiwanda hicho.

“Kenya imejipanga kujenga Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Afrika Mashariki hapa Lamu, na tutahitaji vijana 60,000 kushiriki katika mradi huo,” amesema Rais Ruto.

Rais amesema tayari amefanya mazungumzo na Mfanyibiashara wa Nigeria Aliko Dangote kuhusu uwekezaji huo, akibainisha kuwa kiwanda hicho kitahudumia soko la Kenya pamoja na mataifa mengine ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kulingana na Rais, bidhaa za mafuta zitakazozalishwa katika kiwanda hicho zitasambazwa nchini Kenya na pia katika mataifa ya Ethiopia, Sudan Kusini, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mradi huo unajiri siku chache baada ya Dangote kuthibitisha kuwa Lamu imechaguliwa kuwa eneo la ujenzi wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku.

Kiwanda hicho kinachokadiriwa kugharimu takriban shilingi trilioni 2.2, kinatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya viwanda kuwahi kutekelezwa nchini.

Serikali inaamini kuwa kitasaidia kupunguza utegemezi wa mafuta yaliyosafishwa kutoka nje, kuimarisha usalama wa nishati na kuiweka Kenya kama kitovu cha biashara ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here