Naibu inspekta jenerali wa polisi, Eliud Lagat, amewaagiza makamanda wa polisi kote nchini kuimarisha operesheni dhidi ya magenge ya wahalifu ili kuwahakikishia wananchi usalama.
Lagat alitoa maagizo hayo Ijumaa tarehe 10 Julai 2026 alipokuwa akiongoza kikao cha makamanda wa kanda, na makamanda wa vitengo mbalimbali katika chuo cha mafunzo ya Polisi, ya Kiganjo.
Hili lilijiri wakati ambapo kumeripotiwa msururu wa visa mbalimbali vya uhalifu vikiwemo wizi wa kimabavu hata kwenye maeneo ya umma mchana peupe.
Kikao hicho kiliwakutanisha viongozi wa juu wa huduma hiyo kwa lengo la kutathmini operesheni za kiusalama na kuweka vipaumbele vya siku zijazo.
Akizungumza na makamanda hao, naibu inspekta jenerali alisema lengo kuu ni kuhakikisha kila eneo nchini linabaki salama kupitia operesheni za kiusalama zilizo na uratibu mzuri na zinazotekelezwa kwa uthabiti.
Aliwapongeza maafisa wa polisi kwa umoja wao, uthabiti na weledi waliouonyesha katika kudumisha amani na usalama wakati wa matukio ya hivi karibuni ya kitaifa.
Lagat pia aliwaagiza makamanda kuipa kipaumbele zaidi ustawi wa afya ya akili ya maafisa wa polisi, akisisitiza kuwa ustawi wa maafisa hao ni msingi muhimu wa utoaji wa huduma bora.
Alisema makamanda wana wajibu wa kuhakikisha maafisa wanapata msaada unaohitajika ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na majukumu yao ya kazi.
“Makamanda wanapaswa kuchukua hatua za makusudi na za karibu zaidi katika kusaidia afya ya akili ya maafisa. Ustawi wa maafisa wetu unasalia kuwa nguzo muhimu ya utoaji wa huduma bora,” alisema.
Wakati huo huo, alitaka operesheni dhidi ya magenge ya uhalifu na wasafirishaji wa dawa za kulevya ziendelee kuimarishwa katika maeneo yote ya nchi, akisisitiza dhamira ya Huduma ya Polisi ya kulinda jamii na kudumisha sheria na utulivu nchini.
Huduma ya kitaifa ya polisi zaidi ilitoa hakikisho la usalama wa kutosha kuwezesha mazingira mwafaka ya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Olkalau kwamba kutakuwepo na maafisa wa kutosha kukabiliana na hali yoyote ya uvunjaji sheria baada ya baadhi ya washikadau kulalamikia tuhuma za ukiukaji wa kanuni kuelekea uchaguzi wa Alhamisi tarehe 16 Julai 2026.
Kikao hicho ni sehemu ya mikutano ya mara kwa mara ya viongozi wa huduma ya kitaifa ya polisi inayolenga kutathmini utendaji kazi, kuimarisha uratibu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.









