Inspekta jenerali wa polisi, Idara ya kitaifa ya polisi NPS Pamoja na mwanasheria mkuu wa Serikali Dorcas Oduor wametakiwa kufika mbele ya mahakama kuu ya Kisumu Julai 21, 2026 baada ya kudharau amri za mahakama.
Katika Uamuzi wake Jaji Alfred Mabeya amesema taasisi hizo za serikali zimepuuza maagizo ya mahakama kwa kushindwa kuchapisha kanuni za usimamizi wa mikusanyiko ya umma na matumizi ya nguvu wakati wa maandamano hatua inayokiuka haki ya wananchi ya kufanya maandamano ya amani.
“Hii ni madharau ya utawala wa sheria na ukiukaji wa Kifungu cha 10 cha Katiba. Amri za mahakama si mapendekezo, ni lazima ziheshimiwe na kutekelezwa.” Jaji Mabeya amelekeza.
Mahakama pia imebainisha kuwa vyombo vya dola vilikiuka haki za msingi zinazolindwa na Katiba zikiwemo haki ya kuishi, utu, usawa na usalama wa mtu binafsi.
Mnamo Machi, mwaka 2026 Mahakama kuu ya Kisumu ilitoa fidia ya shilingi milioni 38.6 kwa waathiriwa na familia zilizoathiriwa na ukatili wa polisi wakati wa maandamano jijini Kisumu na kuagiza serikali kuweka kanuni za kudumu za kudhibiti maandamano.
Akizungumza baada ya uamuzi huo Mwenyekiti wa chama cha Wanasheria nchini LSK tawi la Kisumu Dorcas Oluoch amesema ulipaji fidia haupaswi kuwa kisingizio cha kuchelewesha mageuzi akisisitiza kuwa taasisi za serikali zinapaswa kutekeleza kikamilifu maagizo ya mahakama.
“Tuna wasiwasi kwamba kuna juhudi za kuwanyamazisha waathiriwa wa ukatili wa polisi kwa kuwapa fidia. ”
“Tunataka waliohusika wawajibishwe kwa madhara yaliyowapata waathiriwa hao.” Oluoch Amesema.









