Chama cha wanasheria nchini LSK kimetaka uchunguzi wa haraka huru na wa kina ufanyike kuhusu kifo cha Meneja wa huduma za kisheria katika huduma ya misitu KFS Esther Wairimu Keige.
Mwili wa Keige ulipatikana katika shamba la kahawa katika eneo la Juja kaunti ya Kiambu.
Keige mwenye umri wa miaka 54 alitoweka mnamo Juni 10 baada ya kuondoka ofisini kwake kando ya Barabara ya Kiambu Polisi wakisema mwili wake ulipatikana kwenye eneo la Area 4 Karimenu, Juja ukiwa umeanza kuoza.
Jamaa wawili wa wakili huyo walisaidia katika kuutambua mwili huo.
Kulingana na Kamanda wa polisi wa Juja Kombo uchunguzi unaendelea kubainisha chanzo cha mauaji ya Wairimu na mazingira yaliyosababisha kutoweka kwake.
Wanafunzi katika shule moja kwenye eneo hilo waliwaeleza maafisa wa polisi kwamba Wairimu alionekana hivi majuzi akiwa hai shuleni mwao ambapo inaarifiwa kwamba alikuwa akitafta msaada wa chakula kabla ya mwili kupatikana baadaye.
Katika taarifa yake Rais wa LSK Charles Kanjama amesema vifo vya Keige na Wakili Edward Muthee Kariuki aliyeuliwa katika eneo la Athi River Siku chache zilizopita vinazua hofu kubwa kuhusu usalama wa mawakili nchini.
“Ukatili huu usioweza kuelezeka umetokea saa 48 tu baada ya mauaji ya kikatili ya Wakili Edward Muthee Kariuki huko Athi River. Kulengwa na kuuawa kwa makusudi kwa watu wawili mashuhuri katika sekta ya sheria ndani ya wiki moja si tukio la kawaida ni ishara ya vita dhidi ya utawala wa sheria, jaribio la wazi la kuwatia hofu mawakili na dalili ya kutisha kwamba Kenya inaelekea kwa kasi katika kipindi cha uhalifu usiodhibitiwa na kudhoofika kwa taasisi,” Kanjama amesema.
LSK sasa imeitaka Idara ya upelelezi na makosa ya jinai DCI kubuni kikosi huru cha mashirika mbalimbali kuchunguza mauaji hayo, kubainisha wahusika Pamoja na kuwakamata waliotekeleza vitendo hivyo.
“Tunahitaji Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuunda mara moja kikosi huru kinachojumuisha mashirika mbalimbali kuchunguza mauaji, ili kuwabaini kwa kina si tu wahusika waliotekeleza mauaji haya mawili, bali pia waliopanga, waliogharamia na wale wanaonufaika kisiasa au kibiashara,” ameongeza.
LSK pia imetoa wito wa ukaguzi wa faili za ununuzi na ukodishaji na uhamishaji wa ardhi zilizoshughulikiwa na idara ya sheria ya KFS katika miezi 12 iliyopita, kikisema kwamba zoezi hilo litasaidia kutambua maslahi yanayohusiana na kifo cha Keige.
“Tunahitaji ukaguzi kamili na wa uwazi wa uchunguzi wa kisayansi wa faili zote za ununuzi, ukodishaji, na uhamishaji ardhi zinazoshughulikiwa na idara ya sheria ya Huduma ya Misitu ya Kenya katika miezi kumi na miwili iliyopita ili kubaini maslahi mahususi ya kampuni yaliyosababisha kifo cha Wakili Wairimu,” Chama kimesema.
Kanjama ameongeza kuwa vifo vya mawakili wanaohudumia maslahi ya umma vinatishia misingi ya kidemokrasia ya nchi akiapa kuwa LSK itaendelea kusaka uwajibikaji.
Mwili wake unahifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaaa ya chuo kikuu cha Kenyatta ukisubiri upasuaji.









