Washukiwa wanne wa ujambazi wameuawa kwa kupigwa risasi, huku wawili wakitoroka na majeraha ya risasi baada ya kukabiliwa na maafisa wa polisi katika operesheni ya usiku wa kuamkia Jumatatu katika kaunti ya Uasin Gishu.
Kwa mujibu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya saa sita usiku katika barabara ya Eldoret–Kiplombe, baada ya maafisa waliokuwa wakishika doria kupokea taarifa za kijasusi kuhusu wanaume sita wenye silaha na waliovalia mavazi yanayofanana na sare za kijeshi, waliokuwa wakiwavamia na kuwaibia wananchi.
Akidhibitisha tukio hilo Kamanda wa polisi kaunti ya Uasin Gishu Wilberforce Sicharani amesema kuwa maafisa wa polisi walifika haraka eneo la Greenfield Junction, ambako waliwakuta watu sita waliolingana na maelezo yaliyokuwa yametolewa.
Kwa mujibu wa Sicharani, polisi waliwaamuru washukiwa hao wasimame na wajitambulishe, lakini inadaiwa walikaidi amri hizo na kufyatua risasi dhidi ya maafisa wa polisi, hali iliyosababisha majibizano makali ya risasi.
“Maafisa walijibu kwa haraka kukabiliana na tishio hilo kwa kuingia kwenye majibizano ya risasi na washukiwa hao wenye silaha. Kutokana na tukio hilo, washukiwa wanne waliuawa, huku wawili wakifanikiwa kutoroka,” Sicharani alieleza.
Alieleza kuwa msako wa pamoja unaowahusisha maafisa kutoka idara mbalimbali za usalama umeanzishwa ili kuwatafuta na kuwakamata washukiwa hao waliotoroka.
Wachunguzi wanaamini genge hilo linahusika na msururu wa matukio ya uhalifu wa kutumia silaha ambalo limekuwa likiwasumbua wakazi wa eneo la North Rift, ikiwemo Eldoret, Kitale, Kapenguria, Nandi na Marakwet.
Upekuzi uliofanywa katika eneo la tukio ulisababisha kupatikana kwa vifaa mbalimbali vinavyoaminika kutumika katika shughuli za uhalifu.
Polisi walipata bastola moja iliyokuwa na risasi, nyundo maalumu na patasi ya kuvunjia milango, simu tano za mkononi, kamba za manila, vitambulisho vinne na kiasi kisichobainishwa cha fedha.
Operesheni hiyo ni miongoni mwa juhudi za hivi karibuni za polisi za kukabiliana na magenge ya wahalifu wenye silaha yanayoendesha shughuli zao katika eneo hilo, huku operesheni za kuimarisha usalama dhidi ya uhalifu wa kutumia nguvu zikiendelea.
Katika taarifa yake, Huduma ya Kitaifa ya Polisi imesisitiza kujitolea kwake kulinda maisha na mali ya wananchi kupitia operesheni zinazoongozwa na taarifa za kijasusi pamoja na doria endelevu.
Polisi wamewahimiza wananchi kuendelea kuwa macho na kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kwa wakati zinazoweza kusaidia kuzuia uhalifu na kuwakamata washukiwa, huku wakiahidi kwamba taarifa zote zitashughulikiwa ipasavyo wakati uchunguzi ukiendelea.









