IEBC Yaahirisha Kwa muda Usiojulikana Hukumu Katika Kesi Inayomkabili Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia.

0

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imehairisha uamuzi katika kesi inayomkabili mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia kuhusu madai ya kukiuka kanuni za maadili ya uchaguzi.

Tume hiyo ilistahili kutoa uamuzi huo Julai 6 ila imesema itatoa uamuzi huo katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

Muhia anatuhumiwa kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa uliofanyika katika eneo la Olkalau Kaunti ya Nyandarua hatua inayodaiwa kukiuka masharti yanayosimamia mwenendo wa kisiasa katika shughuli za uchaguzi.

“Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kupitia Kamati yake ya Utekelezaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, imeahirisha utoaji wa hukumu katika kesi inayomhusu Mheshimiwa Wanjiku Muhia, Mbunge wa Kipipiri, hadi tarehe inayofuata itakayowasilishwa kwa wakati unaofaa. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa,” tume ilisema.

Kesi hiyo imevutia hisia za kisiasa na kisheria baada ya mawakili wa Muhia kuondoka kwenye kikao cha kusikiliza kesi hiyo wiki iliyopita wakipinga muundo wa kamati hiyo.

Mawakili hao walidai kuwa kesi hiyo ilipaswa kusikilizwa na mwenyekiti wa IEBC Erastus Edung Ethekon Pamoja na Naibu wake Fahima Arafat.

Hata hivyo IEBC ilipinga pingamizi hilo na kuendelea kusikiliza kesi hiyo ikisema kamati hiyo imeundwa kisheria na kwamba ina mamlaka kamili ya kutekeleza kanuni za maadili ya uchaguzi.

“Kikao hiki ni sehemu ya agizo la Tume la kuhakikisha kufuata Kanuni za Maadili ya Uchaguzi na kukuza michakato ya uchaguzi ya amani, halali na inayoaminika,” IEBC ilisema.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here