Aliyekuwa Rais wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo ameonya dhidi ya Ghasia za kisiasa na magenge ya uhalifu yanayoendelea kushuhudiwa nchini.
Ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka ili kukabili hali hiyo.
Katika taarifa yake Odhiambo ametaja kisa cha Ujambazi na wizi katika mkahawa mmoja eneo la Westlands jijini Nairobi kuwa Ishara ya tatizo kubwa la usalama wa kitaifa linalohitaji kuangaziwa kikamilifu.
Amelihusisha tukio hilo na mbinu ya wanasiasa ya kuwatumia vijana na wahuni wakati wa mikutano ya kisiasa kuvuruga amani.
“Ujambazi katika mkahawa mmoja huko Westlands ni matokeo ya miaka mingi ya kuhalalisha matumizi ya wahuni na silaha katika mikutano ya kisiasa,” Odhiambo amesema.
Kulingana na Odhiambo Pindi vijana wanapopewa silaha kwa madhumuni ya kisiasa silaha hizo hazitumiki kwenye mikutano ya kisiasa pekee bali pia kwenye maeneo ya umma.
“Mara tu unapowapa vijana silaha kwa madhumuni ya kisiasa, silaha hizo hazitumiki tu kwenye mikutano ya kisiasa.” ameongeza.
Aidha ameonya kuwa iwapo hali hiyo haitakabiliwa basi huenda ikawa mbaya zaidi kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.









