Wafanyikazi wa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) wametii amri na kusitisha mgomo wao uliodumu kwa siku tatu.
Mgomo huo umesitishwa siku moja baada ya mahakama ya kutatua mizozo ya kikazi kuwaagiza wafanyikazi hao kusitisha mgomo na kurejea kazini mara moja kufuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani na usimamizi wa hospitali hiyo.
Mgomo huo umeathiri pakubwa huduma za matibabu na kusababisha kifo cha mgonjwa mmoja na kuondolewa kwa wagonjwa katika hospitali hiyo.
Hayo yanajiri baada ya tume ya kuratibu mishahara ya wafanyikazi wa umma SRC kusema kuwa haitawapa wafanyikazi hao nyongeza ya mishahara pasipo kufanya utathmini wa utendakazi wao na kwamba tayari walipata nyongeza ya mishahara yao wanayoilalamikia mwaka wa 2017/2018 hadi 2020/2021.








