Kesi ambapo chama cha Thirdway Alliance kinataka mahakama kutoa agizo linalomlazimisha rais Uhuru Kenyatta kuufanyia kazi ushauri wa jaji mkuu David Maraga wa kulivunja bunge chini ya siku 21 itasikilizwa na jopo la majaji.
Jaji wa mahakama kuu James Makau ameagiza faili ya kesi hiyo kupelekewa kwa jaji mkuu kubuni jopo la majaji zaidi ya mmoja kwa sababu inaibua maswala yenye uzito wa kikatiba.
Kupitia wakili wake Elias Mutuma, chama hicho kinahoji kuwa ushauri huo wa Maraga ni sharti utekelezwe chini ya siku 21 na rais hafai kuupuza.
Chama hicho kwenye ombi lake vile vile kinataka ufafanuzi wa mahakama hiyo ya kikatiba kuhusu aina ya uchaguzi utakaoandaliwa iwapo bunge litavunjwa.
Kwa mujibu wa chama hicho, kuvunjiliwa kwa bunge kutasababisha kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo katika kila eneo bunge na wala sio uchaguzi mkuu ambapo wabunge watakaochaguliwa watahudumu katika muhula wa miaka mitano.