Rais Uhuru Kenyatta ameomboleza kifo cha aliyekuwa waziri Simeon Nyachae akimtaja kama kiongozi aliyechangia pakubwa katika maendeleo ya taifa la Kenya.
Katika ujumbe wake, rais amesema hatua ya Nyachae kufaulu kujitenga na siasa na kisha kujiunga na sekta ya biashara iliashiria ukweli wa msemo kwamba bidii hulipa.
Huku akiifariji familia yake, rais amesema kifo kimelipokonya taifa hili kiongozi mwenye busara na ambaye huduma yake kwa taifa imefanya Kenya kupiga hatua kiuchumi ikilinganisha na mataifa mengine.
Rais Kenyatta amesema ilikuwa ni rahisi kumpata kwa mawaidha alipokuwa mbunge wa Nyaribari Chache.
Kwa upande wake, naibu rais William Ruto amemtaja Nyachae kama kiongozi ambaye hakuwa na ubinafsi na aliyehudumia taifa hili kwa ujasiri na kujitolea.
Naye kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amesema jamii ya Abagusii na Kenya kwa ujumla imempoteza kiongozi aliyekuwa na bidii.
Gavana wa Kakamega Wycliff Oparanya, seneta wa Baringo Gedion Moi ni miongoni mwa viongozi wengine walimuomboleza Simeon Nyachae.