Rais Uhuru Kenyatta yuko nchini Uganda kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais Yoweri Museveni.
Rais Kenyatta anahudhuria hafla hiyo kama rais wa Kenya na vile vile katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Marais wengine wanaohudhuria hafla hiyo ni Samia Suluhu wa Tanzania, Paul Kagame (Rwanda), Felix Tshisekedi (DRC), Mohamed Abdullahi Farmaajo (Somalia), Alpha Condé (Guinea) na Nana Akufo Addo (Ghana).
Rais Museveni ataiongoza Uganda kwa miaka mengine mitano, ikiwa ni muhula wake wa sita madarakani.
Aliingia madarakani Januari 1986 kwa mapinduzi ya kijeshi, hadi utakapofika uchaguzi mwingine 2026 atakuwa madarakani kwa miaka 40, sawa na miongo minne wakati huo akiwa na umri wa miaka 81.
Museveni alishinda uchaguzi wa Januari mwaka huu kwa kuwabwaga wagombea wengine kumi katika nafasi ya urais kwa ushindi wa asilimia 58 ya kura zote.