Tatizo la uhaba wa mafuta linaloshuhudiwa katika baadhi ya vituo vya mafuta nchini limetatuliwa na sasa hali imerejea shwari vituoni humo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi amesema kuwa uhaba huo wa muda ulisababishwa na hitilafu za kiufundi zilizoathiri usambazaji wa bidhaa za mafuta miongoni mwa baadhi ya kampuni za uuzaji wa mafuta.
“Wizara ya Kawi inataka kujulisha umma kwamba changamoto za muda za upatikanaji wa mafuta zilizoonekana katika baadhi ya vituo vya mafuta katika maeneo tofauti ya nchi zilitokana na hitilafu za kiufundi na kiutawala.” Waziri Wandayi amefafanua.
Kulingana na Wandayi, uhaba huo ulitokea katika vituo vichache vya mafuta katika maeneo tofauti nchini, akisisitiza kuwa halikuwa uhaba wa kitaifa kama ilivyodhaniwa na baadhi ya Wakenya.
Aidha amesema serikali imechukua hatua za haraka na kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta ili kurejesha hali ya kawaida ya usambazaji.
“Serikali imejitolea kuhakikisha kuwa tunadumisha usalama wa kawi na usambazaji wa mafuta kwa majumba, bishara na viwanda nchini.” Wandayi amedokeza.
Mbadi ameongeza kuwa juhudi za kuongeza upatikanaji wa mafuta tayari zimeanza katika maeneo yaliyoathirika, huku akieleza matumaini kuwa hali ya kawaida itarejea kote nchini kufikia mwisho wa siku.
Wakenya walikumbana na uhaba wa mafuta mwezi jana wauzaji wa bidhaa hio muhimu wakilaumu kufungwa kwa Mkondo wa Hormuz kwa uhaba huo.









