Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko atajitetea mbele ya bunge la Senate kati ya Disemba 17 na 18 baada ya bunge la kaunti ya Nairobi kuidhinisha hoja ya kumbandua mamlakani.
Gavana huyo anakabiliwa na shutma mbalimbali ikiwemo;
*Kudharau bunge la kaunti ya Nairobi kwa kushindwa kutekeleza maamuzi yaliyofanywa na bunge hilo na kusababisha kuongezeka kwa madeni ya kaunti.
*Matumizi mabaya ya afisi na kukiuka sheria za ununuzi pamoja na matumizi mabaya ya pesa za kaunti.
*Kupeana baadhi ya majukumu kusimamiwa na serikali kuu huku akidai kuwa alidanganywa kutia sahihi makubaliano. Na hata baada ya kupeana majukumu hayo, Sonko anatuhumiwa kuvuruga utendakazi wa NMS kwa kukataa kupeana stakabadhi zinazohitajika.
*Gavana huyo vile vile anadaiwa kuwanyanyasa wadogo wake kwa kuwatishia kufanya anavyotaka la sivyo atawafuta kazi na hata kukosa naibu.
*Sonko anadaiwa kutumia mamlaka yake visivyo kutumia pesa za mlipa ushuru kugharamia usafiri wa bintiye hadi mjini New York, Marekani kuhudhuria kongamano la Wanawake mwaka 2018.
*Kesi ya ufisadi inayomuandama Sonko haijaachwa nyuma kwani bunge la kauntyi ya Nairobi linahoji kwamba kuzuiliwa kwake na mahakama kuingia afisini kumefanya vigumu yeye kuwajibikia majukumu yake kama gavana.