Wizara ya afya imeagiza mamlaka ya kununua na kusambaza vifaa vya matibabu KEMSA kuanza kupeana vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya corona kuanzia siku ya Ijumaa.
Akihojiwa na wanachama wa kamati ya bunge la seneti kuhusu afya chini ya uenyekiti wa seneta Michael Mbito, katibu mkuu katika wizara ya afya Dr. Mercy Mwangangi amesema wameagiza KEMSA kuuza vifaa hivyo kwa bei nafuu.
Hatua hiyo huenda ikawa afueni kwa wahudumu wa Afya ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa magwanda ya kujikinga na virusi vya corona wanapokuwa kazini.
KEMSA inatazamiwa kukadiria hasara ya shilingi billion mbili iwapo vifaa hivyo vitauzwa kwa bei ambayo imeelekezwa na wizara ya Afya.
Yakijiri hayo
Kikao cha kamati ya bunge la kitaifa kuhusu Afya kutafuta suluhu la mgomo wa wahudumu wa afya kimeairishwa hadi Alhamisi hii.
Mwenyekiti wa kamati hiyo na mbunge wa Muranga Sabina Chege anasema watahakikisha kuwa maslahi ya wahudumu hao wa afya yanalindwa vema ili warejee kazini kuwahudumia wananchi ambao wanaumia.
Miongoni mwa wale ambao watahudhuria kikao hicho ni maafisa kutoka wizara ya Afya, baraza la magavana, wizara ya hazina ya kitaifa na maafisa kutoka tume ya kuratibu mishahara ya watumishi wa umma SRC kujadili mgomo wa wahudumu wa afya unaoendfelea.
Wakati uo huo
Wauguzi katika kaunti arobaine na nne wameendelea na mgomo kushinikiza kupewa haki zao ikiwemo kulipwa mishahara kwa wakati na kupewa vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukzii yavirusi vya corona.
Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini KNUN Seth Panyako anasema katika kaunti tatu zilizosalia, wauguzi wamedinda kuenda mgomo kwani viongozi hao wameshirikiana na serikali kuwanyanyasa.