Tahadhari ya Mvua Kubwa Yatolewa Katika Maeneo Mbalimbali Nchini

0

Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga kwa mara nyingine imetoa tahadhari kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mvua kubwa katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Machi 3 hadi Machi 9,2026.

Kulingana na idara hiyo, mvua inayotarajiwa kunyesha itakuwa ya viwango vya zaidi ya milimita 20, huku kiwango hicho kikitarajiwa kuongezeka kati ya Jumatano, Machi 4 na Machi 7.

Hata hivyo, mvua hizo zinatarajiwa kupungua kufikia Jumapili, Machi 8 2026.

Idara hiyo aidha imeeleza kuwa licha ya mvua kupungua katika maeneo mengi baada ya Machi 8, mvua ya zaidi ya milimita 20 itaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya bonde la Ziwa Victoria, sehemu za Nyanda za Kati, Nyanda za Kusini Mashariki na ukanda wa Pwani hadi Machi 9.

Kaunti ambazo mvua inatarajiwa kushuhudiwa ni pamoja na Turkana, Samburu, Migori, Nyamira, Bungoma, Busia, Kakamega, Vihiga, Pokot Magharibi, Baringo, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Nandi, Uasin Gishu, Nakuru, Siaya, Kisumu, Homa Bay, Kisii, Kericho na Bomet.

Kaunti za Kiambu, Embu, Murang’a, Kirinyaga, Nyandarua, Nyeri, Laikipia, Tharaka Nithi, Meru, Nairobi, Kajiado, Narok, Makueni, Machakos, Taita Taveta, Kitui, Kwale, Mombasa, Tana River, Kilifi, Isiolo, Marsabit, Garissa na sehemu za Wajir na Mandera pia zikitarajiwa kushuhudia mvua hizo.

Wakazi katika maeneo hayo wamehimizwa kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa mafuriko ya ghafla, kujaa kwa mito na barabara kukatika. Idara hiyo imewataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuepuka kuvuka mito au maeneo yaliyofurika maji ili kuepusha madhara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here