Mamlaka ya Nyanja za ndege nchini (KAA) imekana taarifa kuwa kampuni ya Adani ndiyo mkandarasi wa mradi uliopangwa wa upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Kupitia taarifa Jumanne tarehe 3 Machi 2026, KAA ilifafanua kuwa kampuni hiyo ya India haikuwa imehusishwa katika mradi huo wa mabilioni ya fedha kufuatia kufutiliwa kwa pendekezo lake la mradi wa awali mwaka wa 2024.
‘‘KAA ingependa kufafanua taarifa iliyochapishwa kwenye mojawapo ya magazeti ya leo kuhusiana na kuhusika kwa Adani Group katika upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA),’’ alieleza kaimu afisa mkuu mtendaji wa KAA Dr. Mohamud Gedi.
Mamlaka hiyo aidha ilitoa hakikisho kuwa mradi huo utafadhiliwa na serikali kulingana na sheria.
‘‘Uboreshaji na upanuzi wa JKIA ni mradi unaofadhiliwa na serikali ya Kenya na kutekelezwa kwa mujibu wa kanuni zilizopo za sekta ya umma,’’ aliongeza Dr. Mohamud.
KAA ilitoa taarifa hiyo kufuatia madai kuwa juhudi zilikuwa zikiendelezwa kudumisha ushirikishwaji wa bilionea Gautam Adani katika mradi huo licha ya kufutiliwa mbali kwa mpango wa awali na rais William Ruto.









