Muchina apata uteuzi baada ya kukosa uchaguzi Ol Kalou

0
Rais William Ruto (kulia) pamoja na Samuel Muchina baada ya kukutana.

Rais William Ruto amemteua Samuel Muchina Nyaga, kuwa mwanachama wa Tume ya Mito ya Nairobi, siku chache baada ya kushindwa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Ol kalou kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Muchina, aliyepata kura 5,450 katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, alishindwa na Sammy Kamau Ngotho wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, aliyepata kura 35,440.

Kupitia tangazo la gazeti rasmi la serikali lililochapishwa Jumatano tarehe 22 Julai 2026, rais Ruto alitangaza kuwa uteuzi wa Muchina ulianza kutekelezwa kuanzia siku ya chapisho akichukua nafasi ya Amos Chege Mugo, ambaye uteuzi wake ulifutwa.

“Taarifa inatolewa kwa umma kwamba mimi, William Samoei Ruto, rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, namteua Samuel Muchina Nyaga kuwa mwanachama wa Tume ya Mito ya Nairobi, kuanzia tarehe 22 Julai, 2026,” taarifa hiyo ya gazeti rasmi la serikali ilisema.

Uteuzi huo ulifanyika siku moja baada ya kiongozi wa taifa kukutana na Muchina katika Ikulu jijini Nairobi, ambapo wawili hao walifanya mazungumzo kufuatia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Muchina alisema kuwa ingawa ushindi wao uliahirishwa, dhamira yao ya kuwatumikia wakazi wa Ol Kalou bado ulikuwa thabiti akidokeza kuwa rais alikuwa amempa jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya serikali inayoendelea katika eneo bunge hilo.

Aliongeza kuwa uongozi haukuhusiana tu na kushika wadhifa bali kusimama na wananchi na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wote.

Tume ya Mito ya Nairobi ina jukumu la kuratibu urejeshaji, ukarabati na usimamizi endelevu wa Bonde la Mto Nairobi kwa kushirikisha taasisi za serikali ya kitaifa na zile za kaunti katika uhifadhi wa mazingira na uboreshaji wa maeneo ya mijini.

Aidha, tume hiyo itahakikisha sheria na kanuni zinazohusu mazingira ndani ya bonde hilo zinafuatwa, pamoja na kuandaa miongozo ya maadili kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kwa ushirikiano na wadau mbalimbali.

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ulivutia hisia za kitaifa na ulitazamwa kama mtihani wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, David Kiaraho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here