Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kangema, Martin Kinyua Mutegi, amezuiwa kutekeleza majukumu yake rasmi huku Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) ikianzisha hatua za kinidhamu dhidi yake kufuatia madai ya kupokea hongo.
Hakimu huyo alikamatwa pamoja na Afisa mkuu wa uangalizi wa wahalifu (Probation Officer) wakidaiwa kuitisha na kupokea hongo ya shilingi elfu mia moja na sabini ili kushawishi uamuzi wa kesi ya jinai
Katika taarifa yake, Jaji Mkuu Martha Koome amesema madai yanayomkabili hakimu huyo ni mazito na yakithibitishwa, yatakuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria, Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Mahakama, pamoja na misingi inayozingatia utoaji wa haki.
“Kutokana na hali hiyo, Idara ya Mahakama na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) zimeanza taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Huduma za Mahakama pamoja na sera husika za rasilimali watu. ”
“Hadi taratibu hizo zitakapokamilika, afisa huyo wa mahakama atasimamishwa kutekeleza majukumu yake ya kimahakama kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa, bila kuathiri uchunguzi unaoendelea na taasisi husika za kikatiba.” Koome amesema.
Tukio hili linajiri wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu madai ya maafisa wa mahakama kuhusika katika vitendo vya ufisadi nchini, hali iliyochangia Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kususia shughuli za mahakama kote nchini tarehe 22 Julai, 2026.
Jaji Mkuu Martha Koome amesema mahakama inapaswa kuongozwa na misingi ya kikatiba ya uadilifu, kutopendelea upande wowote, uwajibikaji, uwazi na utawala wa sheria.
Amesema kitendo chochote kinachodhoofisha imani ya umma katika utoaji wa haki kinahatarisha msingi wa Idara ya Mahakama.
“Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara kwamba majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi wa Idara ya Mahakama hawawezi kutoa haki kwa mkono mmoja huku wakitenda uhalifu kwa mkono mwingine.”
“Waliokabidhiwa jukumu la kusimamia utoaji wa haki wana wajibu mkubwa zaidi wa kuheshimu sheria na kuonyesha uadilifu wanaoutarajia kutoka kwa wengine. Ingawa kila anayekabiliwa na tuhuma ana haki ya kufuata mchakato wa kisheria, Idara ya Mahakama haitawalinda wala kuvumilia vitendo vya uhalifu au ukiukaji wa maadili.” Koome amesisitiza.
Amewahakikishia wakenya kuwa Idara ya Mahakama na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) zitaendelea kushirikiana kikamilifu na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na mashirika mengine ya uchunguzi katika kutekeleza wajibu wao wa kikatiba.
“Ninawahakikishia Wakenya kuwa Idara ya Mahakama na Tume ya Huduma za Mahakama JSC zitaendelea kulinda uadilifu wa mfumo wa utoaji haki, na zitachukua hatua thabiti, za haki na zisizo na upendeleo dhidi ya jaji, afisa wa mahakama au mfanyakazi yeyote atakayekiuka viwango vya juu vya maadili vinavyotarajiwa kwa wanaosimamia utoaji wa haki.” Ameongeza Koome.









