Chuma Chenu Ki Motoni Rais Ruto Awaonya Wahuni.

0

Rais William Ruto amesema serikali haitaruhusu magenge ya uhalifu na wahuni kutumia maandamano kuvuruga amani.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi Rais wakati wa uzinduzi wa ripoti mpya ya taifa itakayoifanya Kenya kufikia kiwango cha mataifa bora kiuchumi duniani, Rais amezielekeza asasi za usalama kuchukua hatua dhidi ya wahalifu hao kwa mujibu wa sheria.

Ameongeza kuwa maandamano ya amani ni haki ya kikatiba, ila vitendo vya uhalifu vinavyofanywa kwa kisingizio cha maandamano havitakubalika.

“Nimekuwa nikifuatilia mjadala huo. Maandamano ni haki ya kidemokrasia na halali, lakini pia kuna wahalifu, wahuni na watu wanaoharibu mali za watu na kuiba” Ruto amesema.

Amesema taifa linahitaji mazungumzo ya wazi kuhusu uhalifu, utawala wa sheria na usalama wa nchi.

“Tunahitaji kufanya mazungumzo ya wazi kuhusu uhalifu, utawala wa sheria na usalama wa taifa letu,” amesema.

Rais Ruto pia amekosoa namna baadhi ya washukiwa wa uhalifu wanavyoshughulikiwa mahakamani, akisema baadhi huachiliwa kwa masharti nafuu na baadaye kujihusisha na uhuni katika mikutano ya kisiasa.

“Baadhi ya watu wanaokamatwa kwa makosa ya kihalifu, hupelekwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana ya Shilingi 200.” Rais ameongeza.

Aidha, amezitaka asasi za usalama kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria ili kukabiliana na uhalifu na kulinda mustakabali wa Kenya.

“Sasa kwa kuwa tumefikia mwafaka, vyombo vyetu vya usalama lazima vitekeleze majukumu yake kwa kuzingatia sheria. Lazima vitekeleze majukumu yake na kukomesha uhalifu. Hivyo ndivyo tutakavyolinda mustakabali wa Kenya,” alisema Rais.

Kiongozi wa Taifa pia ametaja umuhimu wa kulinda amani, akionya kuwa mataifa yanaweza kupoteza maendeleo ya miaka mingi pale utawala wa sheria unapodhoofika akilitaja taifa la Sudan kama mfano wa athari za mizozo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here