Rais Atoa Wito Wa Maridhiano Kwa Upinzani Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2027.

0

Rais William Ruto ametoa wito kwa viongozi nchini kuweka kando siasa na kuanzisha mazungumzo ya kitaifa yatakayolenga mustakabali wa Kenya badala ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza kwenye Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema taifa linahitaji mazungumzo ya kina, ya uwazi na yanayowashirikisha Wakenya wote ili kuweka dira ya maendeleo ya muda mrefu.

“Ni lazima tuwe na mazungumzo ya kina kama taifa kuhusu mustakabali wa Kenya. Hii si kuhusu uchaguzi ujao; hii ni kuhusu mustakabali wa Kenya,” Rais amesema.

Amesisitiza kuwa uchaguzi utapita, ila mustakabali wa taifa utasalia kuwa muhimu kwa kila Mkenya bila kujali atakayeshinda au atakayeshindwa.

“Uchaguzi wa mwaka ujao utakuja na kupita. Yeyote atakayeshinda au kushindwa katika uchaguzi huo ataendelea kuwa hapa. Hakuna atakayeondoka nchini. Mustakabali wa Kenya utakuwa na umuhimu kwa kila mtu wale watakaoshinda na wale watakaoshindwa,” alisema.

Aidha, Rais ametoa wito kwa viongozi kuwa wazalendo, waadilifu na wenye kuwajibika katika kushughulikia masuala ya kitaifa.

Amewataka viongozi wa serikali na upinzani kushirikiana katika mazungumzo yenye kujenga taifa ili kuimarisha umoja, amani na maendeleo ya taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Kadhalika Mkuu wa Nchi amewatahadharisha Wakenya dhidi ya kupuuza umuhimu wa amani na utulivu nchini, akitolea mfano wa mzozo unaoendelea nchini Sudan akisema mji wa Khartoum ulikuwa miongoni mwa miji yenye kuvutia miaka michache iliyopita ila sasa umeharibiwa kutokana na machafuko.

Rais amehitimisha kwa kutoa wito kwa viongozi wa serikali na upinzani kukumbatia mazungumzo, akisema ustawi wa Kenya unategemea umoja, kuishi kwa amani na kujitolea kwa pamoja.

“Ningependa kuwaomba viongozi wa upinzani na wale wa serikali tukumbatie mazungumzo. Tofauti za kisiasa zisigeuke chanzo cha migawanyiko, bali ziwe fursa ya kupata suluhu zinazojenga taifa. Kenya ni kubwa kuliko maslahi yetu binafsi au vyama vyetu vya kisiasa, na mustakabali wake unategemea umoja na amani.” alisema Rais.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here