Kenya hugongewa 5% ya pato barabarani

0

Ajali za barabarani zinaigharimu Kenya takriban asilimia 5 ya pato lake la taifa (GDP) kutokana na upotevu wa uzalishaji, gharama za matibabu, huduma za dharura, uharibifu wa mali na ulemavu wa muda mrefu.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) Nashon Kondiwa ameeleza Jumanne tarehe 21 Julai 2026 katika mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuboresha usalama barabarani duniani uliofanyika jijini New York nchini Marekani.

“Tunatambua kuwa mzigo unaotokana na majeraha ya ajali za barabarani bado uko juu kwa kiwango kisichokubalika. Watumiaji wa barabara walio katika hatari zaidi, hasa wanaotembea na waendesha pikipiki, wanachangia idadi kubwa ya vifo, huku makundi haya mawili yakichangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vinavyotokea kwenye barabara zetu.’’ Kondiwa alieleza.

”Ajali za barabarani si suala la uchukuzi pekee, bali pia ni suala la maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kenya inakadiria kuwa ajali za barabarani hugharimu uchumi asilimia 5 ya pato la taifa kila mwaka kutokana na upotevu wa uzalishaji, gharama za matibabu, huduma za dharura, uharibifu wa mali na ulemavu wa muda mrefu,” aliongeza.

NTSA ilionya kuwa mzigo huo ungeweza kufikia asilimia 10 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2030 iwapo hali ingesalia ilivyo.

Hilo lilielezwa huku NTSA kwa ushirikiano na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) pamoja na kaunti ya Nairobi, ikiendeleza operesheni iliyolenga kukabiliana na matumizi hatari ya barabara kutoka kwa wanaotembea yaliyohusishwa na mamia ya vifo kila mwaka.

Kutokana na operesheni hiyo watu ishirini na wawili waliokuwa wakivuka barabara kiholela waliripotiwa kukamatwa na kushtakiwa mahakamani Jumanne kwa kuvuka barabara kuu ya Thika, eneo la Allsops, pasipo kutumia vivukio maalum likiwemo daraja la juu.

“NTSA, kwa kushirikiana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi pamoja na Kaunti ya Nairobi, itaendelea kutoa elimu kwa wanaotembea kuhusu matumizi salama ya barabara.” NTSA ilisema.

Walionaswa walikabiliwa na mashtaka ya kuvuka barabara katika eneo lisiloruhusiwa na kuzuia mtiririko huru wa magari kinyume na sheria za trafiki.

Chini ya kanuni za makosa madogo ya trafiki, wanaopuuza kutumia madaraja na vivuko vilivyotengwa wanaweza kutozwa faini kuanzia shilingi 500, huku mahakama ikiwa na uwezo wa kutoa adhabu kubwa zaidi kulingana na mazingira ya kesi.

Operesheni hiyo ililenga wanaovuka barabara kuu zenye njia nyingi licha ya kuwepo kwa madaraja, hali inayowaweka wao pamoja na madereva hatarini kwa kuwalazimisha madereva kufunga breki ghafla au kubadili mwelekeo.

NTSA ilisema zoezi hilo lilikuwa sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuimarisha uzingatiaji wa sheria za barabarani kupitia utekelezaji wa sheria na elimu kwa umma.

Mamlaka hiyo ilisema ushirikiano na wadau mbalimbali ulilenga kuboresha usalama wa wanaotembea na kuhakikisha wanatumia madaraja na vivuko vilivyotengwa.

Hatua hiyo ilijiri huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu idadi ya wanaotembea ambao walikuwa wameangamia katika ajali za barabarani nchini.

Kulingana na NTSA, wanaotembea walichangia vifo 836 kati ya vifo 2,150 vilivyosajiliwa kutokana na ajali za barabarani katika kipindi cha kwanza cha mwaka 2026.

NTSA ilisema walengwa walichangia asilimia 38 ya vifo vyote vilivyotokana na ajali za barabarani kufikia Juni 30.

Mamlaka hiyo ilisisitiza kuwa ushirikiano wa wanaotembea katika kufuata sheria ni muhimu katika kupunguza vifo barabarani, ikiwataka kutumia madaraja na vivuko vilivyotengwa kila wakati.

“Kwa kuwa wanaotembea ndio watumiaji wakuu wa barabara, uzingatiaji wao wa sheria ni muhimu, lazima wajitolee kutumia madaraja yaliyopo na vivuko vilivyotengwa kila wakati.” Mamlaka ilisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here