Serikali yampa Odinga kaburi la ukumbusho

0
Mchoro wa usanifu wa jengo la makumbusho la Raila Odinga huko Bondo.

Ujenzi wa kituo cha ukumbusho wa aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Raila Amollo Odinga umeanza rasmi baada ya familia yake kuwasilisha eneo la kihistoria la mazihara ‘Kang’o ka Jaramogi’ alikozikwa, katika kaunti ya Siaya, kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya, (KDF) ili kutekeleza mradi huo unaodhaminiwa na serikali.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ilihudhuriwa na waziri wa Ulinzi Soipan Tuya Jumatatu tarehe 20 Julai, ikionyesha mwanzo rasmi wa ujenzi wa mradi huo uliokuwa katika hatua ya maandalizi kwa takriban miezi tisa tangu kifo cha Raila Odinga.

Raila Odinga, aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), alifariki dunia Oktoba 15, mwaka 2025, akiwa na umri wa miaka 80, alipokuwa akipokea matibabu maalumu nchini India.

Mnamo Juni 2026, Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, ilianzisha rasmi mchakato wa utekelezaji wa mradi huo kwa kutenga shilingi milioni 30 za kujenga eneo hilo kuwa kumbukumbu ya urithi wa taifa.

Wakati wa hafla hiyo, seneta wa Siaya Oburu Oginga ambaye ni kakake mkubwa Odinga, alikabidhi rasmi eneo hilo la ukoo kwa jeshi la ulinzi mbele ya mwanawe Raila Odinga Junior, ambaye hivi karibuni alitawazwa kuwa kiongozi wa kitamaduni wa familia ya Odinga.

Akizungumza katika hafla hiyo, waziri Tuya aliwaagiza wahandisi wa jeshi kukamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi cha miezi miwili, huku akihakikishia familia kuwa kasi ya ujenzi haingepunguza ubora wa kazi.

“Ninataka kuwahakikishia kabisa familia za Odinga na Jaramogi kwamba ubora wa ujenzi huu hautaathiriwa licha ya muda mfupi uliotengwa kuukamilisha. Jeshi la Ulinzi la Kenya, limejizatiti kikamilifu kutekeleza jukumu hili, na litakamilisha mradi huu ndani ya kipindi cha miezi miwili ijayo.” Alisema Tuya.

Aidha, Tuya alitoa wito wa kudumishwa kwa umoja wa kitaifa na kuwaonya viongozi dhidi ya siasa za mgawanyiko na uchochezi wa kikabila akikipongeza chama cha ODM kwa mchango wake katika kuunga mkono serikali jumuishi.

“Serikali haitawavumilia watu wanaoeneza matamshi ya chuki au kuchochea ukabila nchini. Tunakipongeza chama cha ODM kwa kuweka maslahi ya taifa mbele na kwa kuunga mkono umoja wa kitaifa, hatua ambayo itaiwezesha Kenya kuwa taifa lenye mshikamano na nguvu zaidi,” alisema.

Kwa niaba ya familia, Raila Odinga Junior alisema kituo hicho cha kumbukumbu kingehifadhi historia na mchango wa baba yake kwa taifa, na kuwa mahali ambapo vizazi vijavyo vingeweza kujifunza kuhusu nafasi yake katika historia ya kisiasa ya Kenya.

“Kaburi hili la ukumbusho si jengo la kawaida pekee, bali ni mahali ambapo historia ya Baba itaendelea kusimuliwa kwa vizazi vijavyo. Baba alikuwa na imani kubwa kwa taifa hili, na aliamini kuwa Kenya ni ya kila mmoja wetu,” alisema.

Awamu ya kwanza ya mradi huo itahusisha ujenzi wa kaburi pamoja na sehemu za maonyesho ya baadhi ya mali binafsi za Raila Odinga, ikiwemo magari aliyotumia katika safari yake ya kisiasa.

Mradi huo pia utahusisha ukarabati wa eneo la kumbukumbu alikozikwa Jaramogi Oginga Odinga, babake Odinga na pia makamu wa kwanza wa rais wa kenya, ambapo maeneo hayo mawili yataunganishwa kuwa kituo kimoja cha urithi wa taifa kitakachokuwa na kumbi za historia, maktaba ya utafiti na hifadhi ya kidijitali ya mchango wa familia ya Odinga katika harakati za uhuru na maendeleo ya demokrasia nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here