Serikali yaeleza Utayarifu wake Kupambana na El Niño.

0

Serikali imewahakikishia Wakenya kuwa imejipanga kikamilifu kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha nchini, huku ikiwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kwani maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza yanaendelea.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema serikali inashirikiana na washikadau mbalimbali ili kuimarisha mikakati ya tahadhari, ikiwemo uratibu wa shughuli za kukabiliana na maafa kabla ya mvua hizo kuanza.

“Tusikuwa na tashwishi. Suala hili linaangaziwa kwa karibu. Tunajitayarisha zaidi katika kuhakikisha kwamba tunaweza kudhibiti athari za mvua za El Niño. Tayari tumeshaanza kuwa na vikao na washikadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba mvua hizi hazitatuathiri.” amesema Mwaura.

Katika juhudi za kuwalinda wananchi walio katika mazingira hatarishi, Mwaura amesema serikali imetenga shilingi bilioni 1.8 kupitia Mpango wa Hunger Safety Net, fedha zitakazonufaisha familia 133,484 katika kaunti za Turkana, Mandera, Wajir, Marsabit, Garissa, Isiolo, Samburu na Tana River.

Aidha, amesema serikali imetoa shilingi milioni 587.9 kwa familia hizo ili kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na athari za ukame na mvua.

Mwaura amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha utayari wa taifa dhidi ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mbali na maandalizi ya kukabiliana na maafa, Mwaura ametangaza ushirikiano mpya kati ya Kenya na Marekani unaolenga kuimarisha utekelezaji wa mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).

Amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya nchini.

Pia amefafanua kuwa fedha za Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) zinasimamiwa kikamilifu na serikali, huku kampuni binafsi za teknolojia zikihusika tu katika utoaji wa huduma za kidijitali za malipo kwa mujibu wa sheria.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here