Mgombea wa Chama cha DCP Sammy Douglas ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa eneobunge la Olkalau Kaunti ya Nyandarua kwa kupata kura 35,440 inayoashiria asilimia 83 na kumpiku mwenzake wa Chama cha UDA Samuel Muchina Nyaga ambaye amepata kura 5,450 inayoashiria asilimia 13 katika uchaguzi uliowavutia jumla ya wagombea 9.
Mgombea Wilson Mwaniki Kigwa wa chama cha Jubilee ametangazwa wa tatu kwa kura 198 akifuatwa na Stephen Wanyoike Waithaka wa chama cha National Liberation kwa kura 103.
Kariuki Timothy Kamau wa chama cha People Reinassance amepata kura 51, Edwin Kariri Muchiri wa Chama cha Party of National Unity akipata kura 28 naye Abdullahi Abdi Fattar wa chama cha Federal Party of Kenya akipata kura 19.
Edward Mathenge Mwaniki wa chama cha Kenya Moja Movement amepata kura 16 kisha Rachael Wangui Njoroge wa chama cha Peoples Democratic akipata kura 11.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi Sammy Douglas wa DCP ameelezea furahha yake baada ya kushinda uchaguzi huo na kuwapongeza wakazi wa Olkalou waliosimama naye katika uchaguzi huo akiwashukuru kwa kutokubali kushawishiwa na wapinzani wao.
“Nimefurahi kutangazwa kama Mbunge wa Olkalou Nataka kuwashukuru wakazi wa eneobunge la Olkalou kwa kuniamini, huu ni ushindi mkubwa.” Amesema Sammy.
Vilevile amemshukuru Kinara wake Rigathi Gachagua kwa kumwaminia katika kinyangayiro hicho na kumsaidia kushinda kiti hicho Pamoja na tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Kwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki
Aidha amewataka wapinzani wake walioshindwa katika uchaguzi huo kukubali matokeo.
“Ningependa kuishukuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kazi nzuri waliyoifanya. Mmefanya jambo la kipekee ambalo wengi hawakulitarajia.”
“Kabla ya uchaguzi kulikuwa na nadharia na uvumi mwingi kwamba matokeo hayatatangazwa, na kwamba kungekuwa na uingiliaji wa mchakato wa uchaguzi. Hata hivyo, mmeonyesha weledi, uwazi na kujitolea katika kuhakikisha mchakato ulitendeka kwa amani na matokeo yanatangazwa kwa wakati. Hongereni kwa kazi hiyo nzuri.” Ameongeza.









