Mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama cha UDA katika uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Ol Kalou, Samuel Muchina Nyagah, amedai kuwa kuna watu wanaotoa hongo kwa wapiga kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kutekeleza haki yake ya kimsingi ya Kupiga Kura katika Shule ya Msingi ya Huruma, Muchina ameitaka mamlaka husika kufuatilia madai hayo na kuchukua hatua zinazostahili ili kulinda uadilifu wa uchaguzi
“Nimesikia kuhusu tukio ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitoa pesa katika vituo vya kupigia kura, na ninatoa wito kwa IEBC kuchunguza suala hilo. Nimearifiwa na watu wangu kwamba kuna baadhi ya watu walikuwa katika vituo vya kupigia kura wakijaribu kuwahonga wapiga kura katika vituo vyetu vya kupigia kura.” Amesema Muchina.
Muchina vilevile amewahimiza wakazi wa Ol Kalou kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Aidha ameonyesha imani kuwa ataibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho, huku akisisitiza kuwa ataheshimu matokeo ya uchaguzi.
“Niko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi huu. Nina imani nitashinda, lakini iwapo matokeo yatakuwa tofauti, niko tayari kuyaheshimu na kuyakubali.” Ameongeza.
Wakati uo huo Muchina ameeleza kufurahishwa na hali ya usalama katika vituo vya kupigia kura akisema kuwa usalama umeimarishwa na kwamba hadi kufikia sasa hakuna tukio lolote la ukosefu wa amani lililoripotiwa.
“Usalama umeimarishwa vyema kwa sababu ukiangalia unaona maafisa wa polisi wako kila mahali, kwa hivyo ninaamini hali ya usalama imedhibitiwa.” Amebaini Muchina.









