Mahakama kuu imeidhinisha uhalali wa sheria zinazopiga marufuku umiliki, matumizi na kilimo cha Bhangi nchini baada ya kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na wanachama wa Rastafari waliokuwa wakitaka bhangi itambuliwe kuwa sehemu yao ya ibada yao ya kidini.
Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Bahati Mwamuye mahakama kuu imesema jumuiya hiyo haikuwasilisha Ushahidi wa kutosha kudhibitisha kuwa sheria hiyo inakiuka Katiba au inapaswa kubatilishwa.
Jaji Mwamuye amesema kuwa ingawa Katiba inalinda Uhuru wa Dini, Imani na Maoni, haki hizo zinaweza kuwekewa mipaka pale inapohitajika kulinda afya ya umma, usalama na maslahi ya wakenya.
“Tunapaswa kuwa na mazungumzo ya wazi na ya dhati kuhusu matumizi ya bangi na mwelekeo tunaopaswa kuchukua kuhusu suala hili,” amesema Jaji Mwamuye.
“Hili si suala linalohusu jamii ya Rastafari pekee. Ni suala la kitaifa linalogusa nyanja zote za jamii yetu,” ameongeza.
Kutokana na uamuzi huo sheria ya kudhibiti dawa za kulevya itaendelea kutumika.
Hii inamaanisha kuwa umiliki, utumizi ukuzaji na uuzaji wa bhangi utaendelea kuwa makosa ya jinai humu nchini Kenya.
Katika sheria hiyo anayepatikana na bhangi atahukumiwa kifungo cha hadi miaka 10, faini au adhabu zote mbili kulingana na uamuzi wa mahakama.









