Serikali imeweka mikakati kukabili ucheleweshaji wa ufadhili wa Elimu ya juu.
Akihojiwa na Kamati ya Bunge la kitaifa ya Uhasibu wa Umma kuhusu utawala na elimu, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba amehusisha hilo na hatua ya Wizara ya Fedha kuchelewesha kusambaza fedha hizo zinazohitajika kufadhili vyuo vikuu na vya kiufundi.
Kulingana na Waziri Migos, Serikali pia inalenga kukabili ucheleweshaji huo kwa kutumia bajeti ya ziada ili kuziba pengo linalosababishwa na bajeti finyu ya elimu.
Hoja kuu ni iwapo vyuo vikuu vinapata ufadhili wa kutosha na unaokidhi mahitaji yao. Serikali itachukua hatua za kuboresha uchakataji na utoaji wa fedha zilizoidhinishwa kwa wakati ili kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aidha amesema wizara ya elimu sasa inapendekeza fedha zote za ufadhili wa elimu kuwekwa katika hazina moja kama mojawapo ya mbinu za kukabili ucheleweshaji na kupungua kwa mgao wa fedha za ufadhili wa elimu.
Ameongeza kuwa wizara hiyo itawasilisha bungeni mswada unaolenga kuwezesha hilo ili kuhakikisha ufadhili kamili wa elimu katika ngazi zote.
“Kwa sasa tumekamilisha Mswada wa Ufadhili wa Elimu ya Juu wa mwaka 2025, ambao unaelekea bungeni. Mswada huo unatoa mapendekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili hatimaye kutatua kabisa changamoto hii.”
Kuhusiana na hali ya sasa ya vyuo vikuu vya umma kuporomoka kutokana na usimamizi mbaya na uhaba wa fedha za kutosha kuviendesha, Waziri Migos amekariri kuwa serikali haitaruhusu vyuo hivyo kuporomoka.
“Tulipoingia madarakani, tulikuta takriban vyuo vikuu 23 vikiwa katika hali mbaya ya kifedha kiasi kwamba vilikuwa karibu kushindwa kujiendesha. Kutokana na mfumo mpya wa ufadhili uliowekwa ili kuhakikisha fedha zinawasilishwa kwa vyuo kwa wakati, tumefanikiwa kupunguza idadi hiyo hadi kufikia takriban vyuo vikuu 11.”









