Aliyekuwa Afisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Peter Mugure Mwaura, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe Joyce Syombua mwenye umri wa miaka 31, na watoto wao wawili binti yao Shanice Maua mwenye umri wa miaka 10, na mwanao Prince Michael mwenye umri wa miaka 5.
Akitoa hukumu hiyo katika Mahakama Kuu ya Milimani Jumanne Julai 14, 2026, Jaji Martin Muya ametaja mauaji hayo kuwa ya Kikatili na kwamba uzito wa kosa hilo unastahili adhabu ya juu zaidi ya kifungo.
“Nimebaini kuwa vitendo vilivyotekelezwa vilikuwa vya kikatili. Kwa kuzingatia kwamba mshtakiwa amekuwa akitumikia miaka kadhaa kizuizini, namhukumu kifungo cha maisha,” amesema Jaji Muya.
Mahakama imebaini kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka kwamba Mugure alimuua mkewe na wanawe wawili, kabla ya kuficha miili yao katika kaburi eneo la Thigithu, Nanyuki.
Jaji Muya amesema ushahidi uliowasilishwa mahakamani, ulionyesha kuwa mauaji hayo yalipangwa kwa makusudi.
Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mugure aliieleza mahakama kuwa hakubaliani na uamuzi huo, huku akiarifiwa kuhusu haki yake ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika Mahakama ya Rufaa.
Kesi hiyo imekuwa miongoni mwa kesi zilizotikisa taifa kutokana na mauaji ya familia yaliyotekelezwa katika Kambi ya Jeshi la Anga Nanyuki.









