Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amemshutumu vikali kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, kwa matamshi yake ya kuwahimiza watalii na wawekezaji kujiepusha na Taifa la Kenya akidai kuwa hali ya usalama nchini imezorota.
Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Mwaura amesema kauli hizo zinaweza kuharibu taswira ya Kenya kimataifa, kudhoofisha imani ya wawekezaji na kuathiri sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa taifa.
“Tunaskia viongozi wengine wa kisiasa wakisema kwamba watu wasusie utalii hapa Kenya kwa kisingizio kwamba hakuna usalama.”
“Utalii ni sekta muhimu zaidi humu nchini kwa hiyo siyo uzalendo. Utalii ni sekta ambayo inatupatia kipato kikubwa zaidi. ” Mwaura amesema.
Mwaura amesisitiza kuwa sekta ya utalii humu nchini inaendelea kuimarika na kuwa imeendelea kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya fedha za kigeni nchini, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha usalama na kuunga mkono ukuaji wa sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Mwaura idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka milioni 1.48 hadi milioni 2.2, huku utalii wa ndani ukifikia watalii milioni 5.2.
Amesema serikali itaendelea kuimarisha usalama na kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha ukuaji huo unaendelea.
Kauli ya Mwaura inajiri siku moja baada ya Gachagua kuwataka watalii na wawekezaji kujiepusha na taifa la Kenya, akidai kuongezeka kwa utovu wa usalama na kuilaumu serikali kwa kushindwa kukabiliana na hali hiyo.
“Imekuwaje wahuni wamechukua udhibiti wa Ol Kalou? Kwa hivyo, Kenya si salama kwa utalii wala kwa wawekezaji. Lakini sisi Wakenya hatuna mahali pengine pa kwenda. Ninyi watalii, ni afadhali msije ili msiumizwe. ” Alisema Gachagua.
Wakati uo huo, Mwaura ametoa wito kwa Wakenya kukataa siasa za migawanyiko na kuendeleza mshikamano wa kitaifa bila kujali tofauti za kisiasa au kikanda.
Amesema serikali imejizatiti kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa usawa, huku akiwahimiza wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuendelea kushirikiana na serikali.
“Tuwe na Umoja tusiingie katika misingi ya ukabila, tusiondoke katika serikali hii serikali ni yetu si ndio tuliipigania tukamchagua Rais Ruto, tutatoka serikali tuende kutafuta nyingine huko msituni? ” Ameongeza Mwaura.









