Kaunti za Maeneo Kame Kunufaika Zaidi na Uwekezaji wa NIF, Asema Kindiki.

0

Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki amesema sehemu kubwa ya rasilimali kupitia Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu (NIF) itaelekezwa katika maeneo kame (ASAL) kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kubadilisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Akizungumza katika sherehe za Sikukuuu ya Madaraka Kindiki amesema uwekezaji huo utasaidia kufanikisha miradi muhimu ya miundomsingi ikiwemo barabara ambazo kwa muda mrefu zimekuwa changamoto katika baadhi ya kaunti za maeneo hayo.

“Nataka nikupongeze mheshimiwa Rais kwa sababu umesema kwamba vile umeanzisha hazina ya kitaifa ya Miundombinu NIF umetuambia kwa ile pesa mingi ya kujenga mabwawa ya maji, rasilimali nyingi zitaelekezwa katika maeneo kame na nusu kame (ASAL), na hiyo itaibadilisha hali ya Wajir na Kaskazini mwa Kenya.” Amesema Kindiki.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza pengo la maendeleo kati ya maeneo mbalimbali nchini na kuimarisha usawa wa kiuchumi.

Wakati uo huo, Kindiki amekanusha madai ya ubaguzi katika ugawaji wa rasilimali za maendeleo akisisitiza kuwa miradi ya serikali inatekelezwa kwa usawa katika sehemu zote za nchi bila kuzingatia misimamo ya kisiasa au kikabila.

“Ninataka kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuchukua msimamo wa ujumuishi na usawa wa nchi yetu. ”

“Mheshimiwa Rais, haujaleta tu heshima kwa watu wote wa Kenya bali pia umeweka mbele ajenda ya ujumuishi kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo ya nchi yetu inagawanywa kwa usawa.” Kindiki Amesema.

Kindiki pia ametaja utoaji wa vitambulisho vya kitaifa kama moja ya hatua ambayo serikali imechukua hatua kuhakikisha hakuna jamii inayotengwa.

“Umetoa utaratibu ambao ulikuwa unawabagua wananchi kutoka sehemu hii ya Kaskazini mwa Kenya na sasa utaratibu wa kutoa stakabadhi za kitaifa zikiwemo vitambulisho unatumika hapa Wajir.” Ameongeza Kindiki.

Amesema wakazi wa maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yakilalamikia changamoto za kupata vitambulisho sasa wanaendelea kuhudumiwa kama Wakenya wengine wote.

Amesisitiza kuwa serikali ya Rais William Ruto imejizatiti kuhakikisha maendeleo yanafikia kila sehemu ya nchi kwa usawa huku ikitoa kipaumbele kwa maeneo yaliyosalia nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here