Waziri wa Afya Aden Duale ametetea mpango wa ujenzi wa kituo cha karantini cha kuwatibu raia wa Marekani wanaoambukizwa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC katika kambi ya Kijeshi ya Laikipia.
Akizungumza katika Bunge la Kitaifa Duale amesema kituo hicho hakina tofauti na vituo vingine vya karantini vilivyowekwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kukabiliana na dharura za kiafya.
“Kituo kinachopendekezwa cha matibabu na kutenga wagonjwa wa Ebola katika Kambi ya kijeshi ya Laikipia ni sehemu ya vituo 23 kama hivyo vinavyopangwa kuanzishwa nchini kama sehemu ya maandalizi ya serikali dhidi ya milipuko ya magonjwa ya kuambukiza. ” Amesema Duale.
Kwa mujibu wa Duale, Mkataba wa ushirikiano kati ya Kenya na Marekani kuhusu kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza yalitiwa saini wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Rais Mstaafu Barack Obama, kabla ya kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
“Kenya na Marekani zilitia saini makubaliano ya ushirikiano kuhusu kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza tarehe 24 Julai 2015 wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta nchini Marekani chini ya uongozi wa Rais Barack Obama, makubaliano hayo yakiidhinishwa na baadaye kuwasilishwa Bungeni mnamo Julai 19, 2016 kwa ajili ya kuzingatiwa. ” Amefafanua Duale.
“Baada ya kupitia taratibu zote pamoja na ushirikishi wa umma, Bunge liliidhinisha makubaliano hayo tarehe 9 Februari 2017 na kuanza kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, ushirikiano huo ulianzishwa upya na kuanza kutumika tena rasmi tarehe 5 Aprili 2022. ” Ameongeza Duale.
Aidha, Duale amesema kuwa kufikia sasa kenya haijarekodi kisa chochote cha Ugonjwa wa Ebola akiongeza kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na mlipuko wowote wa Ebola na kusisitiza kuwa vituo vya karantini vimetengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ningependa kuihakikishia Bunge hili na wananchi wa Kenya kwamba Taifa halijarekodi kisa chochote kilichothibitishwa cha ugonjwa wa Ebola kufikia tarehe 3 Juni 2026. ”
“Katika ngazi ya kitaifa, Hospitali ya Kenyatta imeandaa kitengo cha kutenga na kutibu wagonjwa chenye vitanda 8 kwa ajili ya maandalizi ya dharura. ” Duale ameeleza.
Wakati uo huo amesema kuwa kaunti 12 nchini zimeorodheshwa kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya Ebola kutokana na nafasi ya Kenya kuwa kitovu cha usafiri wa biashara nchini.
Akizungumza Bungeni Duale amesema kuwa kaunti ya Nairobi, Mombasa, Kiambu, Uasin Gishu, Busia, Transnzoia, Nyeri, Nakuru, Nyamira, Pokot Magharibi, Turkana, Homabay, Migori, Kisii, Kisumu na Bungoma ziko katika kaunti zenye hatari ya juu zaidi kupata maambukizi hayo.
Amesema kuorodheshwa kwa kaunti hizo kuwa kwenye hatari kunatokana na shughuli nyingi za usafiri wa watu na bidhaa kupitia ukanda wa usafiri wa Northern Corridor unaounganisha Kenya na mataifa jirani.
Nyingine ni Vihiga, Kakamega, Nakuru, Kericho, Nandi, Kiambu, Machakos, Kilifi, Makueni, Taita Taveta, Isiolo, Garissa na Elgeyo Marakwet.









