Wakenya wengi hawana Imani na taasisi muhimu za kitaifa, zikiwemo Ofisi ya Rais, Bunge, Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na Mahakama, haya ni kulingana na utafiti mpya wa shirika la TIFA.
Ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi tarehe 4 Juni, 2026, inaonyesha kuwa Bunge ndilo linaloongoza kama mojawapo ya Taasisi ambazo wakenya hawana Imani nayo.
“Imani ya wananchi inaendelea kuwa dhaifu katika taasisi zote kuu, huku kukiwa na mashaka makubwa kuhusu ufanisi, uwajibikaji na utoaji wa huduma,” inasema ripoti hiyo.”
Matokeo hayo yanatokana na utafiti wa kitaifa uliofanywa kati ya Mei 2 na Mei 11, 2026, ukihusisha wakenya 2,013 kutoka kaunti zote 47 nchini.
Matokeo yanaonyesha kuwa katika taasisi zote zilizotathminiwa, viwango vya wananchi kutokuwa na Imani vilizidi vile vya kuaminiwa, ikimaanisha kuwa Wakenya wengi walieleza kuwa hawana imani kabisa ikilinganishwa na wale waliodai kuwa na imani kiasi.
Kulingana na ripoti hiyo, Bunge linaongoza likirekodi asilimia 72 ya wakenya wasio na imani tofauti na asilimia 27 ya walio na Imani, ikifuatiwa na Idara ya Polisi iliyorekodi asilimia 29 ya wakenya walio na Imani tofauti na asilimia 69 ya wakenya wasio na imani.
Rais William Ruto pia alipata asilimia 29 ya wakenya wanaomwamini tofauti na asilimia 68 ya wakenya ambao hawamwamini.
Vyama vya kisiasa vimerekodi kiwango sawa cha asilimia 29 ya kuaminiwa na asilimia 68 ya kutoaminiwa.
Viongozi wa serikali za kaunti walipata asilimia 31 ya kuaminiwa na asilimia 67 ya kutoaminiwa, sawa na kiwango hasi cha asilimia 36.
Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC ilifuata kwa karibu ikiwa na asilimia 30 ya kuaminiwa na asilimia 66 ya kutoaminiwa.
Kwa upande wake Idara ya Mahakama imeonekana kufanya vyema zaidi ikilinganishwa na taasisi nyingine, asilimia 60 ya wakenya wakisema hawana imani kabisa na idara hiyo huku asilimia 36 ya wakenya wakionyesha Imani yao na idara hiyo.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa hakuna taasisi iliyopata imani kubwa ya umma.









