Hakuna likizo ya mapema; wizara ya Elimu yasisitiza.

0

Wizara ya Elimu imetangaza kuwa kalenda ya shule kwa muhula wa pili haitabadilishwa licha ya visa vya machafuko katika baadhi ya taasisi za elimu.

Akizungumza na wanahabari Jumatano tarehe 10 Juni 2026, waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alisema kuwa visa vya machafuko vimeripotiwa katika shule za sekondari za juu 204 pekee, huku asilimia 98 ya shule zikiendelea kuwa tulivu na kuendesha shughuli zake kama kawaida.

Waziri Ogamba alibainisha kuwa masomo katika shule za msingi na shule za sekondari msingi yameendelea bila kukatizwa, na hakuna usumbufu mkubwa ulioripotiwa.

Ogamba alisema kuwa mbali na changamoto zilizoshuhudiwa katika baadhi ya shule za bweni za sekondari za juu, mfumo wa elimu unaendelea kufanya kazi vizuri, na kwa hivyo, wizara itaendelea kuzingatia kalenda ya shule iliyopitishwa, ambapo mapumziko ya katikati ya muhula yamepangwa kuanza Juni 24 hadi Juni 28, 2026.

“Machafuko haya yanaonekana kusababishwa na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na changamoto za uongozi katika taasisi za elimu, wasiwasi wa wanafunzi na msongo wa mawazo unaohusiana na mitihani, mazingira duni ya shule, hasa katika sehemu za mabweni, matumizi ya pombe na dawa za kulevya, ratiba ngumu za shule, pamoja na ushawishi wa marika na tabia ya kuiga wengine, ambapo wanafunzi wanadai kuruhusiwa kwenda nyumbani mapema,” alisema Ogamba.

Shinikizo lilikuwa likiongezeka kwa wizara kubadilisha kalenda ya shule na kuwaruhusu wanafunzi kuanza mapumziko ya katikati ya muhula mapema.

Hii ilifuatia kuripotiwa kwa machafuko katika shule kadhaa za sekondari za juu, ambapo baadhi ya shule zilichomwa moto na miundombinu mingine kuharibiwa.

Wizara hiyo ilitangaza mipango ya kufanya marekebisho katika kalenda ya shule kuanzia mwaka ujao wa masomo ili kuhakikisha mihula ya shule inakuwa na uwiano mzuri na kwamba muhula wa pili unafupishwa.

Tukio la uchomaji moto katika shule ya sekondari ya juu ya wasichana ya Utumishi Academy huko Gilgil, kaunti ya Nakuru, tarehe 28 Mei 2026, liliripotiwa kusababisha vifo vya wanafunzi 16 na kujeruhi wengine 79.

Wasichana tisa wanaoshukiwa kuhusika na kuanzisha moto huo walifikishwa katika mahakama ya Naivasha, ambayo iliamuru wazuiliwe katika kituo cha watoto cha Nakuru kwa siku 21.

Waziri wa Elimu alisema kuwa vitendo vyovyote vya ukiukaji wa sheria shuleni vitashughulikiwa kwa ukali akiwataka wakuu wa shule kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa wakati ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa wanafunzi unadumishwa.

Akizungumza katika jumba la Jogoo jijini Nairobi, waziri Ogamba aliagiza shule kuimarisha hatua za usalama, kuboresha programu za mwongozo na ushauri nasaha, na kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kabla ya mwisho wa mapumziko ya katikati ya muhula.

Ogamba alidokeza kwamba wizara itaunda timu ya wadau mbalimbali kuchunguza sababu za machafuko hayo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.

Wazazi wamehimizwa kutumia mapumziko ya katikati ya muhula kuwalea na kuwaongoza watoto wao kuwa raia wenye maadili mema na wanaoheshimu sheria.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here