Oburu apendekeza marekebisho sheria ya maandamano

0

Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Oburu Oginga, ametoa wito wa kufanyiwa marekebisho kwa sheria zinazosimamia maandamano na migomo ya amani.

Amesema kuwa wakenya hawapaswi kulazimika kuomba ruhusa ya polisi kabla ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuandamana.

Akizungumza katika ikulu jijini Nairobi siku ya Jumatatu wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mfumo wa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu, Oburu alisema mfumo uliopo unapaswa kurekebishwa ili kubainisha wazi kwamba waandamanaji wanatakiwa tu kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu nia yao ya kuandamana badala ya kuomba kibali.

Alisema kuwa polisi wanapaswa kuwa na jukumu la kuwezesha maandamano kwa kutoa ulinzi kwa waandamanaji badala ya kuamua iwapo wanaweza kutekeleza haki waliyopewa na Katiba.

“Watoe tu taarifa, si kuomba kibali. Unawapa taarifa na wao wanakupatia ulinzi, na unaeleza mahali utakapoandamana na muda wa kuanza na kumaliza ili usalama uweze kutolewa,” alisema.

“Nilidhani kuna utaratibu kama huo, lakini kama haupo basi tuuharakishe kuuweka ili tuwe na sheria inayosimamia maandamano na kuwawezesha wakenya kuandamana kwa amani bila kuvurugwa.”

Oburu alisema kuwa wakenya, ambao hulipia Huduma ya Kitaifa ya Polisi kupitia kodi zao, wanastahili kulindwa wanapotumia haki zao za kikatiba.

Alilaani matukio ambapo maandamano yameishia kwa majeraha na vifo kufuatia makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.

“Wakenya ndio wanaolipa polisi; basi polisi walindwe na wakenya ili wawalinde, si kuwaua. Risasi inayotumika inanunuliwa kwa fedha za mwananchi unayemuua, kwa hivyo hatupaswi kuruhusu hali kama hiyo kuendelea,” alisema.

Licha ya katiba kumhakikishia kila mtu haki ya kukusanyika, kuandamana, kufanya migomo ya amani na kuwasilisha maombi kwa mamlaka za umma, inataka shughuli hizo kufanyika kwa amani na bila kubeba silaha.

Oburu alisisitiza umuhimu wa kuzingatia masharti hayo, akionya kuwa uwepo wa watu wenye silaha mara nyingi huharibu uhalali wa maandamano na kutoa sababu ya kutumika kwa vurugu.

“Wakenya wanapokwenda kuandamana kwa amani, hawapaswi kubeba panga, mawe au silaha yoyote. Ukiona mtu amebeba kisu au jiwe, ujue huyo ni mhuni,” alisema.

Mwanasiasa huyo mkongwe pia alielezea wasiwasi wake kuhusu kile alichokitaja kuwa kuzoeleka kwa vurugu za kisiasa kupitia matumizi ya magenge ya kukodiwa.

Kulingana naye, wanasiasa kutoka pande mbalimbali za kisiasa wamekuwa wakiajiri makundi ya watu ili kuvuruga mikutano, maandamano na shughuli nyingine za umma.

“Wahuni hao ni wengi; karibu kila mwanasiasa siku hizi ana kundi la wahuni wa kukodiwa kuvuruga shughuli za wengine. Lazima tuhakikishe utamaduni huo wa uhuni wa kisiasa unakomeshwa kabisa,” alisema.

Oburu alizungumza mbele ya rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome, wanachama wa mahakama, watetezi wa haki za binadamu, viongozi wa kisiasa na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali.

Ripoti iliyozinduliwa inalenga kuweka mfumo wa kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu wa kihistoria na wa sasa kupitia fidia na hatua nyingine za kurejesha haki, wakati mjadala wa kitaifa kuhusu uwajibikaji, mwenendo wa polisi na ulinzi wa haki za msingi ukiendelea.

Katika taarifa yake, Oburu alisema mpango wa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu ulikuwa miongoni mwa masuala yaliyopiganiwa kwa muda mrefu na mtangulizi wake, Raila Odinga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here