Serikali imeonya kuwa Kenya bado iko katika hatari kubwa ya kukumbwa na mlipuko wa virusi vya Ebola licha ya kutokuwa na kisa chochote kilichothibitishwa hadi sasa ikitaja ongezeko la mienendo ya watu kati ya mataifa jirani yanayopambana na virusi hivyo.
Katibu mkuu wa idara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, amesema kuwa Kenya inaendelea kuimarisha ufuatiliaji na hatua za maandalizi huku visa vya Ebola vikiendelea kuripotiwa katika mataifa jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.
Muthoni alisema kuwa DRC imerekodi visa 635 vya Ebola huku Uganda ikiripoti visa 18, hali inayoongeza hatari ya maambukizi kuvuka mipaka.
“Ni lazima tuendelee kuwa waangalifu sana kuhusu ugonjwa wa Ebola kwa nguvu zote, kwa sababu Kenya bado iko katika hatari kubwa na katika hali ya tahadhari ya juu kutokana na mienendo mikubwa ya watu kati ya Kenya, DRC na Uganda,” alisema Muthoni.
Hata hivyo, wizara ya Afya iliwahakikishia wakenya kuwa hakuna kisa chochote cha Ebola kilichokuwa kimeripotiwa nchini ikisisitiza kuwa imeanzisha hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa kisa chochote kinachoshukiwa kinagunduliwa na kudhibitiwa kwa haraka.
“Ingawa kwa sasa Kenya haina kisa chochote cha Ebola, timu zetu za kukabiliana na dharura lazima ziendelee kuwa tayari wakati wote,” alisema.
Onyo hilo linajiri wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki kuhusu uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huo hatari wa kuambukiza, ambao husambazwa kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au vitu vilivyochafuliwa na virusi hivyo.
Maafisa wa afya wameimarisha ufuatiliaji katika maeneo ya kuingia nchini, ikiwemo viwanja vya ndege na vituo vya mpakani, huku timu za dharura zikiendelea kuwa tayari kuchunguza na kushughulikia visa vyovyote vinavyoshukiwa.
Muthoni amewataka wahudumu wa afya na wananchi kwa ujumla kuwa macho na kuripoti mara moja dalili zozote zinazoshukiwa, akisisitiza kuwa maandalizi ndiyo silaha muhimu zaidi ya nchi dhidi ya mlipuko wowote unaoweza kutokea.
Ebola ni ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi vinavyowaathiri binadamu na nyani, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo mara nyingi husababisha vifo usipokabiliwa mapema.
Dalili zake hujitokeza ghafla na zinaweza kujumuisha homa, uchovu, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kutapika, kuendesha na, katika baadhi ya visa, kutokwa damu mwilini.









