Rais Akabiliwa na Tishio la Hoja ya Kuondolewa Madarakani.

0

Serikali imetakiwa kusitisha mara moja ujenzi wa kituo cha karantini kinachopendekezwa kujengwa Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Katika taarifa, Baraza la Haki na Usawa likiongozwa na Mwenyekiti wake Sebastian Onyango, limeitaka serikali kueleza kwa uwazi madhumuni ya mradi huo, msingi wake wa kisheria, tathmini za afya na mazingira pamoja na kiwango cha ushirikishwaji wa wananchi kabla ya utekelezaji wake.

“Wananchi wa Kenya wana haki ya kikatiba ya kupata taarifa, kushiriki katika mchakato wa ushirikishwaji wa umma, kulindwa kwa mazingira yao na kuongozwa kwa uwazi katika maamuzi yanayowahusu,” imesema taarifa hiyo.

Baraza hilo limesisitiza kuwa miradi inayohusisha vimelea hatari vya magonjwa lazima izingatie viwango vya juu vya uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa umma.

“Miradi inayohusisha vimelea hatari vya magonjwa inapaswa kuzingatia viwango vya juu vya uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa umma. Chochote kilicho chini ya hapo kinadhoofisha imani ya wananchi,” imeongeza taarifa hiyo.

Aidha, baraza hilo limeikosoa serikali kwa kile ilichokitaja kuwa kupuuza maagizo ya mahakama yaliyositisha ujenzi wa kituo hicho, likisisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa Katiba na mamlaka ya mahakama.

“Pale ambapo mahakama imetoa amri kuhusu mradi huo, maagizo hayo lazima yaheshimiwe na kutekelezwa na vyombo vyote vya serikali bila ubaguzi,” taarifa imeongeza.

Wakati uo huo, Baraza la Haki na Usawa limeeleza wasiwasi kuhusu kile lilichokitaja kuwa kuendelea kwa ubinafsishaji na ugawaji wenye utata wa ardhi ya umma likitaka kufanyika kwa ukaguzi wa kitaifa wa miamala yote inayohusisha ardhi ya umma pamoja na kusitishwa kwa mgao wowote unaobishaniwa hadi uchunguzi huru ukamilike.

Aidha, limeeleza wasiwasi kuhusu maendeleo yanayoathiri Hifadhi ya Mbuga ya Kitaifa ya Wanyamapori ya Nairobi, likisema hifadhi hiyo ni hazina ya taifa yenye thamani kubwa ya kimazingira, kiuchumi na kihistoria ambayo lazima ilindwe.

“Tunatoa wito wa kulindwa kwa Hifadhi ya Mbuga ya Kitaifa ya Wanyamapori ya Nairobi na kufanyika kwa ukaguzi wa kitaifa kuhusu miamala yote yenye utata inayohusisha ardhi ya umma, ikiwemo masuala yanayohusu ardhi ya Chuo Kikuu cha Kenyatta,” ilisema taarifa hiyo.

Baada ya kutathmini kwa kina masuala hayo, baraza hilo limesema limeanza mashauriano na wabunge, wataalamu wa sheria za Katiba, mashirika ya kiraia, viongozi wa kidini na wadau wengine kuhusu hatua za uwajibikaji wa kikatiba dhidi ya maafisa wa umma watakaobainika kukiuka wajibu wao wa kikatiba.

Baraza hilo limesema kuwa iwapo kutapatikana ushahidi wa kuaminika unaoonyesha ukiukaji mkubwa wa Katiba, matumizi mabaya ya mamlaka, kutoheshimu amri za mahakama, kushindwa kulinda rasilimali za umma au kupuuza haki za wananchi, Bunge lina wajibu wa kuchukua hatua bila woga wala upendeleo.

“Tumeanza mashauriano na wataalamu wa sheria za Katiba, mashirika ya kiraia, viongozi wa kidini na wadau wengine kuhusu hatua za uwajibikaji wa kikatiba. ”

“Pale ambapo ushahidi wa kuaminika utaonyesha ukiukaji mkubwa wa Katiba, matumizi mabaya ya ofisi, kutoheshimu amri za mahakama na kushindwa kulinda rasilimali za umma pamoja na haki za wananchi, tutaunga mkono juhudi za kuanzisha mchakato wa kumng’atua madarakani Rais William Ruto kwa mujibu wa Kifungu cha 145 cha Katiba ya Kenya,” ilisema taarifa hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here