Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ametoa onyo kali kwa magenge ya wahalifu na wahuni, akisema kuwa yeyote atakayetiwa mbaroni atakabiliwa kama mhusika binafsi katika kukabili utamaduni wa uhalifu na vurugu nchini.
Akizungumza Jumatano wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la utawala katika kituo cha polisi cha Kiamumbi kaunti ya Kiambu, Kanja aliwaelekeza maafisa wa polisi kuwachukulia hatua kali wale wanaojihusisha na shughuli za uhalifu, akisema kuwa watu wanaojiunga na magenge watawajibishwa kama wahalifu binafsi.
“Mtu yeyote anapoamua kujiunga na magenge na wahuni, atachukuliwa hatua kama mtu binafsi, si kama sehemu ya kundi,” alisema.
Kanja alifichua kuwa washukiwa watano tayari wamekamatwa kuhusiana na shambulizi la hivi karibuni katika kanisa la kianglikana la All Saints Cathedral, lililoko jijini Nairobi na akaonya kuwa watu wengine zaidi wanaohusishwa na uvamizi huo wanaendelea kusakwa.
“Juzi kuna wale walienda kwa kanisa pale. Tumeshika watano. Mtaona katika siku zijazo kukiwa na ukamataji zaidi,” alisema.
Aliwaonya vijana dhidi ya kushawishiwa kujiunga na mitandao ya uhalifu, akisema kuwa kuhusika na magenge kutawaletea majuto wao pamoja na familia zao.
Kanja alisema kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) iko katika safari ya ukumbatiaji mfumo wa kidijitali inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wakenya.
Kanja alisema lengo la huduma hiyo ni kubadilisha vituo vya polisi kuwa vituo vyenye ubora, huku ikiboresha uhusiano kati ya maafisa wa polisi na jamii wanazozihudumia.
“Tuna dhamira ya kuhakikisha kuwa tuna maafisa waliopata mafunzo bora na wenye motisha. Kwa sasa NPS iko katika mchakato wa kuhamia huduma za kidijitali. Hali imefikia hatua ambapo unaweza kuwasiliana na kituo cha polisi ukiwa nyumbani kwako. Lazima tuweke huduma zote za NPS katika mfumo wa kidijitali kwa sababu hatua hiyo itapunguza hongo na ufisadi,” alisema Kanja.
Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa amewaweka viongozi wote wa polisi katika hali ya tahadhari na kumpa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) maagizo makali kuhakikisha wahalifu wanachukuliwa hatua zinazostahili.
“Wahalifu ni wahalifu bila kujali wanatoka upande gani. Ninawasihi, tafadhalini epukeni uhalifu. Kujiunga na wahuni kutawaletea nyinyi na familia zenu mateso makubwa,” aliongeza.
Onyo la Kanja linajiri huku viongozi wa tabaka mbalimbali wakijitokeza kukashifu mchipuko wa magenge ya wahuni yanayoshukiwa kutumiwa na baadhi yao kuvamia mikutano mbali mbali ya hadhara inayoonekana kuwa na ajenda kinzani.









