Rais William Ruto amefafanua kuwa mageuzi ya serikali kuhusu utoaji wa vitambulisho vya kitaifa hayakufuta uhakiki wa uraia, akisisitiza kuwa ni raia halali pekee wa Kenya watakaopatiwa nyaraka hizo.
“Vitambulisho vya Kenya vitatolewa tu kwa raia halali wa jamhuri hii.” Asema Ruto.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka yaliyofanyika Kaunti ya Wajir siku ya Jumatatu, Rais Ruto amesema mageuzi hayo yanalenga kumaliza ubaguzi dhidi ya jamii za Kaskazini mwa Kenya na kaunti za mipakani, na si kudhoofisha taratibu za uthibitishaji wa uraia.
Aidha amesema kwa miaka mingi, wakazi wa maeneo ya Kaskazini mwa Kenya wamekuwa wakikumbana na vikwazo wakati wa kutafta vitambulisho, licha ya kuwa raia wa Kenya kwa kuzaliwa.
Wakati uo huo amesisitiza kuwa Katiba inawapa Wakenya wote haki sawa bila kujali kabila, dini au eneo wanakotoka.
“Kila Mkenya anastahili ulinzi sawa, heshima sawa na kutendewa haki sawa chini ya sheria,” alisema.
Aidha ametaja kuwa mnamo Februari 2025 akiwa Wajir, alitoa amri kuhusu usajili na utoaji wa vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na kaunti nyingine zilizoathirika.
Kwa mujibu wa Rais, hatua hiyo ilimaliza miongo kadhaa ya ubaguzi uliowanyima wananchi wengi upatikanaji wa nyaraka muhimu za utambulisho akiongeza kuwa mageuzi hayo tayari yamewawezesha maelfu ya vijana walio umri wa miaka 18 kupata vitambulisho bila masharti.
“Nisisitize wazi kuhusu kile uamuzi huo haukuwa. Haukuwa mwaliko kwa wageni kupata nyaraka za Kenya kinyume cha sheria,” amesema Ruto.
Ameongeza kuwa serikali imejizatiti kulinda uadilifu wa mfumo wa utambulisho wa taifa na kuhakikisha usalama wa nchi.
“Hatukufuta uhakiki wa uraia. Tulifuta ubaguzi,” Rais amesema.









