Chama cha DCP chamtaka Waziri Murkomen kujiuzulu kwa utepetevu wa kukabili majanga shuleni.

0

Chama cha DCP kinachoongozwa na Rigathi Gachagua kimetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusiana na chanzo cha moto katika shule ya upili ya wasichana ya Utumishi iliyo Gilgil kaunti ya Nakuru.

Hii ni kufuatia mkasa wa moto uliofanyika usiku wa kuamkia Alhamisi tarehe 28, Mei 2026 na kusababisha vifo vya watoto 16 na kujeruhiwa kwa wengine 74.

Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi alasiri katika makao makuu ya chama hicho, Katibu Mkuu John Methu ameitaka Wizara ya Usalama wa ndani kutoa taarifa ya kina kuhusu uwezo wa serikali kukabili majanga.

“Taifa lolote linalopoteza vijana wake katika majanga ambayo yangeweza kuzuiwa lazima lijitathmini kimaadili.”

“Taifa linapoomboleza, tunahoji mikakati ya kukabiliana na majanga nchini haswa katika shule za bweni.”

“Tumepoteza wanafunzi wengi kwa muda mrefu kuanzia mkasa wa St Kizito miaka ya 1990, Hillside Endarasha Academy mwaka 2024.”

Aidha, ameitaka Wizara ya usalama wa ndani kuharakisha Mswada wa Kitaifa wa Usimamizi wa Majanga akisema utasaidia kuzuia au kupunguza matukio kama hayo siku zijazo.

“Inasikitisha kwamba mswada wa kitaifa wa usimamizi wa majanga umekwama chini ya uongozi wa Bunge la Kitaifa, wakati watoto wetu wanaendelea kukabiliwa na hatari mashuleni.”

Aidha, ametaka hatua za nidhamu kuchukuliwa dhidi ya Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba pamoja na kujiuzulu kwa Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen kufuatia tukio hilo.

“Tangu mkasa wa moto wa Endarasha mwaka 2024, hatujawahi kuelezwa jinsi watoto 21 walivyopoteza maisha. Tunaishi katika nchi ya aina gani?”

“Tunataka hatua za haraka za kinidhamu dhidi ya Waziri wa Elimu pamoja na kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen kufuatia vifo vya watoto wetu katika shule ya wasichana ya Utumishi.”

Shinikizo hizo zinajiri wakati serikali ikiendelea na uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here