Huenda shule zote za umma nchini Kenya zikaanza kutumia sare za rangi moja ya kitaifa huku kila shule ikitakiwa kubaki na utambulisho wake kupitia nembo maalum.
Pendekezo hilo linaendelea kuibua mjadala baada ya kutolewa na washikadau wa elimu katika warsha ya elimu mjini Naivasha kwa kusudi la kusuluhisha changamoto zinazokumba utekelezaji wa mfumo wa elimu ya umilisi CBE.
Washikadau hao wanasema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama kwa wazazi na kuimarisha usawa katika shule hasa wakati wa kununua sare.
Pia wamependekeza shule za msingi na zile za sekondari msingi (JSS) ziunganishwe kuwa moja chini ya usimamizi mmoja wa shule na bodi moja ya usimamizi, kwa kuwa na manaibu walimu wakuu watakaokuwa chini ya mwalimu mkuu mmoja.
“Mkutano huo uliamua kwamba nchi inapaswa kupitisha sare za shule zilizo sanifishwa katika ngazi zote za elimu, ili kuimarisha usawa, umoja na uwezo wa kumudu gharama.”
“Hata hivyo, shule zitaruhusiwa kudumisha utambulisho wao wa kipekee kupitia nembo maalum kwenye sare hizo. Aidha, mkutano huo uliamua kuwa gharama za sare za shule zinapaswa kudhibitiwa na kuwekwa kiwango maalum ili kupunguza mzigo wa kifedha kwa wazazi.” imesema maazimio hayo.
Hata hivyo baadhi ya washikadau wanahisi kwamba matumizi ya sare ya rangi moja yanaweza kuleta mkanganyiko wakati wanafunzi kutoka shule mbalimbali wanapokutana katika makongamano au shughuli zingine za pamoja kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Awali Rais William Ruto aliwataka washikadau hao kushughulikia tatizo la gharama za shule akisema limekuwa kikwazo kwa watoto kutoka familia maskini kupata elimu nchini.









