Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imekashifu vikali matamshi ya hivi majuzi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaodai kuwa watahujumu matokeo ya Uchaguzi Mkuu ujao 2027.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Tume hiyo imeeleza madai hayo kuwa yasiyo na msingi na hatari kwa mchakato wa kidemokrasia ikionya kuwa matamshi hayo yanalenga kueneza hofu, kupotosha umma na kudhoofisha imani ya wananchi katika mfumo wa uchaguzi nchini.
“IEBC inakashifu vikali matamshi ya hivi majuzi ya baadhi ya wanasiasa wakidai kwamba wataathiri mchakato wa uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa urais wa mwaka 2027 kupitia njia zisizo za kisheria. Matamshi hayo, yanaweza kupotosha mtazamo wa umma kuhusu michakato ya kidemokrasia nchini Kenya. ”
Tume hiyo aidha imesisitiza kuwa jukumu la kuendesha na kusimamia uchaguzi nchini liko chini ya tume hiyo pekee na haliwezi kuchukuliwa na mtu yeyote, taasisi au mwanasiasa huku ikipuuza madai kuwa Tume hiyo inaweza kushinikizwa, ikisema madai hayo ni ya uongo na ya kupotosha.
Kadhalika tume hiyo imesema itashirikiana na mamlaka husika kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya wale wanaosambaza taarifa potofu kuhusu hujuma za uchaguzi.
Wakati huo huo, IEBC imefafanua kuwa Kanuni ya Maadili ya Uchaguzi kwa sasa bado haijaanza kutekelezwa rasmi kwa sababu hakuna kipindi rasmi cha uchaguzi kilichotangazwa.
Tume hiyo imebainisha kuwa hakuna tangazo rasmi lililotolewa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, jambo ambalo linafanya matamshi ya sasa ya kisiasa kuonekana kuwa ya mapema na yasiyo na uwajibikaji.
” Kanuni ya Maadili ya Uchaguzi kama ilivyoainishwa chini ya Kifungu cha 84 cha Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, pamoja na Kifungu cha 110 cha Sheria ya Uchaguzi, kwa sasa bado haijaanza kutekelezwa rasmi, kwa kuwa IEBC hupatiwa mamlaka chini ya kanuni hiyo wakati wa kipindi rasmi cha uchaguzi. ”
Hata hivyo, IEBC imewahakikishia Wakenya kuwa itaendelea kulinda uhuru wake, kutokuwa na upendeleo pamoja na kutekeleza wajibu wake wa kikatiba.
Tume hiyo pia imewahimiza wananchi kushiriki katika zoezi linaloendelea la usajili endelevu wa wapiga kura na kujiandaa kutumia haki yao ya kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
IEBC imesisitiza kuwa imejizatiti kuhakikisha uchaguzi huo utaendeshwa kwa njia ya wazi na huru kwa mujibu wa Katiba ya Kenya pamoja na viwango vya kimataifa vya uchaguzi.
“IEBC inaendelea kujitolea kikamilifu kuhakikisha kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 utakuwa huru, wa haki. “









