Hakuna aliye juu ya sheria, NCIC yaonya.

0

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imesema haitasita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote atakayepatikana na hatia ya kuvuruga amani nchini.

Akizungumza na wanahabari Mwenyekiti wa NCIC Askofu Kepha Nyamweya ameibua wasiwasi kuhusu kutovumiliana kisiasa, kauli za chuki, na uchochezi wa kikabila unaoshuhudiwa nchini.

Nyamweya amewaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kutumia kauli za uchochezi akisema ushawishi wa kisiasa hautoi kinga dhidi ya uwajibikaji.

“Tume haitakatishwa tamaa na cheo, umaarufu, au ushirika wakati wa kutekeleza mamlaka yake. Mtu yeyote, bila kujali wadhifa wake, atakayepatikana amekiuka Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, 2008, atakabiliwa na hatua kamili za kurekebisha na kutoa adhabu zinazopatikana, ikiwa ni pamoja na mashtaka pale ambapo ushahidi unastahili,” amesema Mwenyekiti wa NCIC.

Tume hiyo aidha imevitaka vyama vya kisiasa kutekeleza nidhamu chamani na kuhakikisha kwamba maafisa wao na wagombea, wanafuata viwango vya kikatiba na kisheria vya maadili katika shughuli zote za kisiasa na mawasiliano.

“Vyama vina jukumu la moja kwa moja la kitaasisi kwa mwenendo wa wanachama wao,” Kepha alisema.

Tume pia imebaini usumbufu kwenye mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya umma, matamshi ya uchochezi kutoka kwa wanasiasa na matamshi kwenye mtandao ya kijamii yanayowalenga watu binafsi kwa sababu ya maoni yao ya kisiasa na kulaani matukio ambayo pia yanatishia demokrasia.

NCIC aidha imehimiza wanasiasa kujizuia na kuonyesha heshima kwa wapinzani wao wa kisiasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here