Tulieni Kutakuwa Sawa Kindiki Awaambia Wakenya.

0

Naibu wa Rais Profesa Kithure Kindiki amewahimiza Wakenya kuwa na subra huku serikali ikiendelea kutafuta suluhu ya changamoto ya ongezeko la bei ya mafuta nchini.

Akizungumza katika eneo la Miseleni-Mwala, Kaunti ya Machakos, Kindiki amelaani vikali visa vya uharibifu wa mali vilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei hiyo, akisisitiza kuwa maandamano yanapaswa kufanyika kwa njia ya amani bila kuhatarisha maisha na mali ya wananchi.

Amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kupunguza makali ya gharama ya mafuta ili kumlinda mwananchi wa kawaida dhidi ya mzigo wa gharama ya juu ya maisha.

Kadhalika amesema kuwa hali ya sasa imechangiwa pakubwa na mzozo unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati kati ya mataifa ya Marekani, Iran na Israeli, hali iliyovuruga njia za usafirishaji wa mafuta duniani.

“Juzi tumeshuhudia misukosuko kutokana na vita vinavyoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati kati ya Marekani, Iran na Israeli. Njia zinazotumika kusafirisha mafuta zimeathirika, lakini nataka kuwahakikishia Wakenya kuwa serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha bei ya mafuta inadhibitiwa ili wananchi wasiathiriwe zaidi.” Kindiki amesema.

Aidha, Naibu wa Rais ameukosoa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa siasa za uchochezi, akisema uchaguzi mkuu ujao unapaswa kuongozwa na sera, maendeleo na rekodi ya utendakazi wa viongozi badala ya propaganda za kisiasa.

“Tutafakari kuhusu maisha yetu, watoto wetu, biashara zetu na shughuli zetu za kila siku. Wakati wa siasa ukifika, wananchi wachague viongozi kulingana na kazi na maendeleo waliyoleta kwa wananchi.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here