Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametoa makataa ya siku 40 kwa serikali kuangazia ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake pamoja na dhulma za kijinsia nchini, yakionya kuwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa basi yatafanya maandamano ya kitaifa.
Katika taarifa iliyotolewa tarehe 20 Mei 2026, mashirika hayo yamewasilisha orodha ya matakwa yao kwa serikali yakitaka hatua za haraka kuchukuliwa, ikiwemo kutangaza dhulma za kijinsia pamoja na mauaji ya wanawake kama janga la kitaifa.
Mashirika hayo pia yanataka kubuniwa na kufadhiliwa kwa hazina maalum ya kusaidia waathiriwa wa dhulma za kijinsia, uwajibikaji zaidi kutoka kwa huduma ya kitaifa ya polisi NPS na uzinduzi wa kampeni ya kitaifa dhidi ya dhulma za kijinsia.
“Ikiwa matakwa haya hayatatekelezwa, itakuwa ishara ya ukosefu wa uwajibikaji na dhamira kutoka kwa wale waliopewa jukumu la kulinda wananchi.”
Wito huo umejiri siku chache baada ya Chama Cha wanasheria nchini LSK pia kuelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la visa hivyo mnamo Mei 13 mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika la FIDA Kenya, visa 35 kati ya 70 ambavyo vimeripotiwa kila wiki mwaka huu vinahusishwa moja kwa moja na dhulma za kimwili na kingono zinazotekelezwa na wapenzi au watu wa karibu.
Aidha, mashirika hayo yametishia kuandaa maandamano ya amani kote nchini iwapo serikali haitachukua hatua zinazohitajika.









