Mswada wa Fedha wa Mwaka 2026 unahujumu asema Matiangi.

0

Chama cha Jubilee kimewahimiza Wakenya kuupinga Mswada wa Fedha wa 2026/2027, kikionya kwamba sheria inayopendekezwa ina vifungu vya adhabu ambavyo inasema vitazidisha gharama ya maisha na kuisukuma nchi katika mgogoro mkubwa zaidi.

Wakizungumza Jumatano wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Naibu Kiongozi wa chama Fred Matiang’I, Katibu Mkuu Richard Kenta na Naibu kiongozi wa chama hicho Jeremiah Kioni wamesema mswada huo utawaathiri zaidi Wakenya wa kawaida ikiwa utapitishwa.

“Sisi kama chama cha Jubilee ndio wa kwanza kusema tunajiunga na wakenya wengine kukataa mswada wa fedha wa mwaka 2026/27 ukiangalia yale ambayo yako kwenye huo mswada unashangaa tutaishi wapi na tunaelekea wapi ” Matiang’I amesema.

Aidha aneongeza kuwa serikali imekataa ukaguzi wa fedha chini ya mpango wa IMF na badala yake imechukua mbinu za muda mfupi katika usimamizi wa uchumi, hatua anayoisema inahatarisha uthabiti wa uchumi wa nchi.

Amesema hali ya juu ya gharama ya maisha inaendelea kuwaumiza wafanyakazi na familia nyingi nchini, akitoa wito wa uwazi zaidi, uwajibikaji na mageuzi katika sekta muhimu kama vile nishati ili kuboresha hali ya uchumi wa wananchi.

“Wafanyikazi wa taifa hili sahii sijui kama kuna mfanyikazi wa nchi hii anatarajia kupata mshahara maisha ya kufanya kazi nchini humu imekuwa kama utumwa. Hii serikali imetoka kwa mpango wa IMF kwa saababu wamekataa kukaguliwa. ” ameongeza Matiang’I.

Wakati uo huo Matiangi amemkashifu waziri wa usalama Kipchumba Murkomen kwa madai kuwa maandamano ya kupinga bei ya mafuta yalichochewa kikabila akisema kuwa matamshi ya Murkomen ni ya uchochezi yanayopanga kuligawanya taifa hili kwa misingi ya kikabila.

” Huezi sema hii shida imeletwa na wakikuyu ama imeletwa na wakamba au na kabila flani hiyo ni tabia ya mtu ambaye ameshindwa kufanya kazi. ” ameongeza.

Kwa upande wake Naibu kiongozi wa chama hicho Jeremiah Kioni amesema maandamano yaliyoshuhudiwa tarehe 18 na 19 Mei 2026, yalikuwa ujumbe kutoka kwa Wakenya kwamba imetosha, akisisitiza kwamba maandamano hayo hayakuchochewa na uhamasishaji wa kisiasa.

“Tulichokiona katika siku mbili zilizopita ni kauli ya Wakenya wakisema imetosha, hakukuwa na kauli hata moja ya kisiasa kabla ya maandamano,” Kioni amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here