Chama cha Jubilee kimeendelea kuikosoa vikali serikali ya Kenya Kwanza kikidai kuwa taifa linaelekea katika msukosuko mkubwa wa kiuchumi.
Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Naibu Kiongozi wa chama Fred Matiang’i wameukashifu uongozi wa sasa wakisema umeshindwa kupunguza gharama ya maisha na kuimarisha hali ya uchumi kwa wananchi wa kawaida.
“Ninaifahamu vizuri serikali hii na ninawaambia Wakenya kwa ukweli kwamba taifa linaelekea katika hali ya hatari kwa sababu linaongozwa na serikali isiyo na uwezo wa kusimamia mambo ipasavyo. Mbali na kutokuwa na uwezo, serikali hii pia imesimamia vibaya rasilimali na uchumi wa nchi.” Matiang’i amesema.
Kwa mujibu wa Matiang’i, viongozi wana wajibu wa kuwasikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zinazowakabili badala ya kutoa matamshi yasiyo na suluhu kwa matatizo ya wananchi.
“Ningependa kuwasihi viongozi wetu wachukue muda sasa kuangazia na kutatua changamoto zinazowakabili Wakenya badala ya kuendelea kutoa kauli zisizowasaidia wananchi.” Matiangi amesema.
Aidha, ameikashifu serikali kwa kuhusisha changamoto za kiuchumi na sababu wanazodai hazina msingi, wakisema wananchi wanaendelea kuumia kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha ikiwemo gharama ya usafiri kufuatia ongezeko la bei ya mafuta.
Matiang’i ameongeza kuwa serikali inapaswa kuwashirikisha wananchi katika maamuzi muhimu yanayohusu uchumi kabla ya kutekeleza hatua zinazoweza kuongeza mzigo kwa wananchi.
“Ni wazi kuwa matamshi yao yanaonyesha namna wanavyojaribu kukwepa uwajibikaji. Wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta bei ya mafuta ilipanda lakini hakukuwa na hali kama hii kwa sababu tulikuwa viongozi wenye kuwajibika, tulizungumza na wananchi na tuliheshimu maoni yao.” Ameongeza.









