Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya amesema kiwango cha ulipaji wa mkopo wa Hustler Fund kimeimarika pakubwa na sasa kufikia asilimia 90.
Akijibu maswali ya maseneta katika Bunge la Seneti, Oparanya amekiri kuwa kiwango cha kutolipa mikopo hiyo kilikuwa juu muda mfupi baada ya mpango huo kuzinduliwa, japo anakariri kuwa kila Mkenya aliyechukua pesa hizo ataandamwa hadi pale atakapozilipa.
“Tumekuwa tukizungumza na wakopaji na ninaweza kuwahakikishia kuwa baadhi yao wameweza kulipa. Tunawahimiza wale ambao bado hawajalipa kufanya hivyo. Na kwa vyovyote vile, kwa wale ambao hawatalipa, iwapo tutachukua hatua za kisheria tunazo nambari zao za vitambulisho. Kwa sasa kiwango cha kutolipa mkopo huo ni cha chini sana.” Amesema Oparanya.
Wakati uo huo, Oparanya ametetea hatua ya serikali kupitia wizara yake kusitisha usajili wa vyama vipya vya ushirika.
Amesema hatua hiyo ililenga kuhakikisha kuna uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa vyama hivyo.
- “Kusitishwa kwa usajili wa vyama vipya vya ushirika (SACCOs) haikuwa kufungia shughuli zao bali ilikuwa mpango wa kimkakati wa kulinda wanachama, kurejesha hadhi ya sekta hiyo na kuweka msingi wa sekta ya SACCO iliyo imara na inayodhibitiwa ipasavyo.” Oparanya ameongeza.









