Gachagua Aibua Madai Mazito Dhidi ya Ruto, Macron na Usalama wa Ukanda wa Afrika Mashariki.

0

Kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua sasa anadai kuwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron yupo nchini kufanya mashauriano kuhusu shilingi bilioni saba zinazofaa kulipwa kwa mashirika ya Ufaransa yaliyofaa kufanikisha ujenzi wa barabara ya Rironi–Mau Summit ila mkataba wao ukafutiliwa mbali.

Kwa mujibu wa Gachagua mashirika hayo yalipewa zabuni ya shilingi bilioni 159 wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kukarabati barabara ya Rironi – Mau Summit lakini zabuni hiyo ikafutiliwa mbali na Rais Ruto na kukabidhiwa kwa mashirika kutoka China.

Kutokana na hatua hiyo mashirika hayo yanafaa kulipwa shilingi bilioni 7 huku Gachagua akimshtumu Rais Macron kwa madai ya kutumia kongamano la Africa Forwad kuwafumba macho wakenya.

“Rais Macron amekuja kufanya mashauriano kuhusu shilingi bilioni 7 wala si kuhudhuria kongamano hilo.” Gachagua amesema.

Wakati uo huo, Gachagua amemhusisha Rais Ruto na ukosefu wa usalama kwenye ukanda wa Afrika Mashariki akisema kuwa viongozi wanaowahangaisha raia kwenye mataifa yanayoshuhudia mapigano wamepewa hifadhi humu nchini.

Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kujitenga na Rais Ruto iwapo analenga kuleta amani na utulivu katika eneo hilo.

“Haiwezekani kuzungumzia amani nchini Sudan huku mwenyeji wa mkutano huo akihusika katika kuchangia ukosefu wa usalama.” Gachagua ameongeza.

Aidha, amedai kuwa ushirikiano kati ya Rais Ruto na waasi wa M23 ulimfanya Rais wa DRC Félix Tshisekedi kutohudhuria kongamano la Africa Forward jijini Nairobi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here